SERIKALI YAOMBA USHIRIKIANO ZAIDI NA BENKI YA DUNIA
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Uchumi
Mpana, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo
katika ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Waziri wa
Fedha na Mipango aliishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kuisaidia
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Joseph
Magufuli katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maedeleo hapa nchini.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa uchumi
wa nchi umeendelea kukua kwa kiwango cha kati ya asilimia 6-7 kwa muda
na hivyo kuiwezesha Serikali kuendelea na utoaji wa huduma za jamii na
kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa pomaja
na nia ya kuendeleza mafanikio mazuri yaliyopatikana katika awamu za
Serikali zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli imedhamiria kwa dhati kujenga uchumi imara kwa kuendeleza
viwanda na kuweka mazingira mazuri ya biashara ili kuvutia wawekezaji wa
ndani na wale wa nje kuja kuwekeza nchini , kujenga miundombinu ya
barabara, reli, umeme , viwanja vya ndege na kuongeza uwekezaji katika
utoaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji.
Aidha, ameeleza kuwa katika
kufikia malengo hayo , Serikali imefanya juhudi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato, kusimamia vizuri
matumizi ya fedha za Serikali, kuongeza bajeti ya maendeleo hadi kufikia
asilimia kati ya 35 na 40 ya bajeti nzimat, kuongeza ufanisi katika
utendaji wa umma na kupambana na rushwa pamoja na mambo mengine.
Pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi,
Dkt. Mpango alisema kuwa Taifa bado linakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, kiwango cha umasikini
bado kiko juu, ukuaji mdogo wa Sekta ya kilimo ambayo imeajiri
takribani asilimia 70 ya watanzania unaosababishwa na ukosefu wa mbegu
bora, miundombinu ya umwagiliaji na soko la uhakika, na kupungua kwa
mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi pamoja na mambo mengine.
Katika kusaidi juhudi za Serikali
kupambana na changamoto mbalimbali , Dk. Mpango aliiomba Benki ya Dunia
kupitia kwa Dk. Felipe kuisadia Serikali mkopo wa Dola za Kimarekani
milioni 150 kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji huduma (
Growth and Service Delivery) amabao uko katika hatua ya maandalizi.
Mkurugenzi wa Uchumi Mpana,
Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo, kwa
upande wake aliipongeza Serikali ya awamu ya tano ya Dk. John Pombe
Joseph Magufuli kwa kazi nzuri inayofanya ya kusimamia uchumi mpana,
kuongeza makusanyo ya ndani ambayo yanasaidia upatikana fedha kwa ajili
ya kugharamia uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kupambana
na rushwa, kusimamia matumizi ya fedha za umma, na kuongeza ufanisi
katika utendaji wa kazi za umma.
Aidha, Dkt. Felipe aliishauri
Serikali kuwekeza zaidi katika rasilimali watu na miundombinu ili
kulifanya Taifa kuweza kuhimili ushindani wa kimataifa dunia na
kujenga uchumi unaokua na endelevu.
Vile vile aliieleza kuwa katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita uwekezaji kutoka nje umekuwa zaidi
katika Sekta ya madini, hivyo alishauri Serikali kuweka mazingira mazuri
ya biashara ili kuwavutia wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika sekta
za viwanda na utoaji huduma ili kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi na
kuchochea ukuaji wake.
Mkurugenzi wa
Uchumi Jumla, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Felipe Jaramilo akifafanua
jambo katika kikao na Waziri wa Fedha na Mipango kilichofanyika Jijini
Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango akizungumza na ujumbe wa Mkurugenzi wa Uchumi jumla,
Biashara na Uwekezaji (hawapo pichani), katika kikao kilichofanyika
Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James akisisitiza jambo katika kikao kati ya Waziri
wa Fedha na Mipango na Mkurugenzi wa Uchumi Jumla, Biashara na Uwekezaji
wa Benki ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia
nchini Tanzania, Bi. Bella Bird na Mkurugenzi wa Uchumi, Biashara na
Uwekezaji, Dkt. Felipe Jaramilo, mara baada ya kikao kilichofanyika
Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizaraya Fedha na Mipango
……………….
Na Benny Mwaipaja, WFM
Post a Comment