WANANCHI WALALAMIKIA MAENDELEO YA KIJIJI CHAO KUKWAMA
KYELA-MBEYA
WANANCHI wa vitongoji vitatu vilivyopo kijiji na
kata ya Ipinda wilayani Kyela mkoani Mbeya,wameiomba halmashauri ya wilaya ya
Kyela mkoani Mbeya kutatua mgogoro uliopo kati ya wenyeviti wa vitongoji na
mwenyekiti wa kijiji ili kuharakisha maendeleo yaliyokwama kwa muda mrefu.
Kijiji cha Ipinda chenye wakazi zaidi ya elfu 10
kina vitongoji vitatu kupitia Chadema ambavyo wenyeviti hao wameingia kwenye
mgogoro na mwenyekiti wa kijiji tangu achaguliwe,hali inayowalazimu wenyeviti
hao wa vitongoji kuwajibika moja kwa moja kwa afisa mtendaji wa kata pasipo
muhtasari wa kijiji.
Akizungumzia hali hiyo jana kwaniaba ya wananchi
wengine,Esrael Kilanga mkazi wa Ipinda,alisema kwa muda mrefu sasa kijiji hicho
kinazidi kudumaa kimaendeleo kutokana na kutoelewana kati ya wenyeviti wa
vitongoji na wa kijiji na kwamba walipeleka malalamiko kwa diwani wa kata ili
awakirishwe kwa mkurugenzi wa halmashauri lakini hadi leo kimya.
Kutokana na hali hiyo alisema wao kama wananchi
wanamuunga mkono mwenyekiti wa kijiji licha ya kuwa wote wanatokana na Chadema
lakini hawako tayari kushirikiana na wenyeviti wa vitongoji ambao wamekuwa
wakifanya kazi pasipo ridhaa yao.
Akithibitisha kuwepo kwa sintofahamu
hiyo,mwenyekiti wa kijiji cha Ipinda Sadat Mwambungu (CHADEMA) ni kweli hali
hiyo ipo na kwamba imetokana na misimamo ya kuwatetea wananchi kwani kabla
hajawa kiongozi kulikuwepo na michango ya mara kwa mara na kandamizi ambayo kwa
sasa amepiga marufuku.
Alisema yeye aliingia madarakani katika uchaguzi
wa mwaka 2014 lakini alifanyiwa vigisu na viongozi wa wilaya na kulazimika
kuondolewa madarakani kwa sababu ya misimamo yake,na kwamba ulipoitishwa
uchaguzi mungine alipita kura nyingi za mtikisiko ambapo hadi sasa anafanyiwa
fitna iliyosababisha afarakane na viongozi wenzake.
‘’Haiwezekani wenyeviti wa vitongoji wachangishe
fedha za maendeleo kwa wananchi pasipo muhtasari wa kijiji na hata kuwasomea
mapato na matumizi,nimezuia michango hiyo,na kibaya zaidi wenyeviti hao
wanawajibika kwa afisa mtendaji na diwani na nimepeleka malalamiko kwa mkurugenzi
lakini hadi leo kimya’’alisema.
Diwani wa kata hiyo Dr,Hunter Mwakifuna
(CCM) licha ya kukiri kuwepo na sakata hilo,alisema hilo ni tatizo la
mwenyekiti wa kijiji kwani amekuwa akifanya mambo yaliyo nje na sheria na
kwamba kwa kufanya hivyo ndiyo maana wenyeviti wa vitongoji wanapoingana na
maamuzi yake.
Dkt,Mwakifuna ambaye pia ni mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya hiyo,alisema mwenyekiti Mwambungu amekuwa hapatani na
baadhi ya wenyeviti na wajumbe kwenye vitongoji kitu ambacho kimekuwa
kikizorotesha maendeleo ya kijiji hicho na kuwa kwakuwa kipo kwenye kata yake
analazimika kupambania maendeleo.
Mkuregenzi mtendaji wa Mussa Mgatta,suala hilo
lipo jikoni linashughulikiwa na kwamba watazungumza na pande zote mbili ili
kupata suruhu itakayoifanya maendeleo ya kijiji hicho yasonge mbele.
Post a Comment