BILIONI 3.7 ZATOLEWA KUKARABATI BARABARA MBEYA
SHILINGI Bilioni 3.7 zimetolewa na Serikali kwaajili
ya ujenzi wa barabara mbalimbali jijini Mbeya kwa kiwango cha lami.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Amos Makalla alibainisha hayo
kwenye uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kipande cha barabara cha kutoka Isyesye
hadi Relini jijini Mbeya chenye urefu wa kilomita 2.3.
Makalla alisema ujenzi wa kipande hicho cha barabara
kitakachonufaisha kata za Isyesye na Itezi utagharimu Shilingi milioni 881.
Alisema Serikali imetenga fedha hizo kwaajili ya
kuendeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami jijini hapa na kurahisisha
shughuli za usafirishaji kupitia miundombinu rafiki.
Aliwapongeza wakazi wa kata ya Isyesye waishio
jirani na barabara kwa ushirikiano walioonesha kwa Serikali kwa kukubali kwa
hiyari kubomoa bila fidia sehemu ya nyumba zilizokuwa ndani ya eneo linalopaswa
kufikiwa na barabara.
“Mmeonesha ushirikiano mkubwa katika mradi
huu.Naamini ni kwakuwa mmetambua nini Serikali inamaanisha hata ikaamua
kuwajengea barabara kwa kiwacho cha lami.Maana kuna watu wengine hata kama
wanapelekewa maendeleo na serikali tena kwa jambo ambalo limekuwa changamoto
kwao kwa muda mrefu wao utawasikia hatutaki mpaka tulipwe fidia.Na wengine hata
wakilipwa fidia bado wanakuwa wagumu.”
“Serikali inapenda watu walio na ushirikiano.Na
ndiyo sababu sisi tumejipanga popote walipo wananchi wanaoonyesha ushirikiano
tutapeleka miradi.Hatutaki watu wanaokaa wakati wote wanafanya siasa hao
tutahamisha miradi”alisisitza Makalla.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Isyesye,Ibrahim
Mwampwani alisema barabara ya lami ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na wakazi
wa kata za Isyesye na Itezi kutokana na adha waliyokuwa wakiipata hususani
nyakati za mvua nyingi.
Alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutakuwa
kichocheo kikubwa cha maendeleo situ kwa wakazi wa kata hizo mbili bali na
maeneo mengine kwakuwa watu wengi wataitumia badala ya kulazimika kupita
barabara kuu pekee.


Post a Comment