MKUU WA MKOA WA MBEYA ATANGAZA VITA NA KIKUNDI CHA WATU WANAO JIITA WAKOREA WEUSI
SERIKALI mkoani Mbeya imetangaza vita dhidi ya kundi
la vijana wanaojiita Wakorea weusi ambao wamekuwa tishio jijini hapa kwa
kuwapiga nondo watu na kasha kuwapora na kuwafanyia vitendo vya ulawiti na
ubakaji.
Kikundi cha vijana wanaojiita wakorea weusi kinachotajwa
kuwa na matawi mbalimbali kimekuwa tishio katika maeneo mbalimbali jijini hapa
na kusababisha watu kuishi kwa hofu kubwa.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla ametangaza vita
dhidi ya vijana hao jana na akisema sasa Polisi wanaingia mtaani kuwasaka na
ole wake atakayekamatwa.
“Sina lugha nzuri ya kuwaambia.Ole wao!Nataka RPC
kuanzia usiku wa leo hao watu wajue siyo salama kwao.Hatuwezi
kukubali,tutawasaka kila kona na tutahakikisha tunamaliza mpaka kiini”
“Mimi kama mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama
ya mkoa hatuwezi kukubali watu wachache wavuruge amani ya mkoa.Watafute kazi
nyingine.Hata kama mko hapa nawaambieni kuanzia usiku wa leo hamko salama.Tunataka
mkoa wetu uwe salama watu wetu wafanye shughuli zao za kimaendeleo katika hali
ya amani na utulivu”alisisitiza Makalla alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata
za Isyesye na Itezi jijini hapa.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliwataka wananchi kutoa
ushirikiano kwa jeshi la polisi akisema kwa vyovyote watu wanojihusisha na
uhalifu huo wanaishi ndani ya jamii hivyo polisi wanaweza kukabiliana nao kwa
dhati kutokana na ushiriki wa wana jamii.
Kwa upande wao Machifu wa kabila la Wasafwa kupitia
kwa Chifu Ally Nyenze walisema vitendo vya upigaji nondo vinavyofanywa na kundi
la wakorea weusi vimekuwa tishio kubwa hususani katika maeneo ya
Isyesye,Itezi,Ilomba,Mama John na Soweto.
Naye Diwani wa kata ya Isyesye,Ibrahim Mwampwani
alisema ni siku tatu tu zimepita tangu mwalimu mmoja apigwe nondo na watu
watatu ambapo kutokana na majeraha aliyoyapata amelazwa katika hospitali ya
Rufaa kanda ya Mbeya anakoendelea kupata matibabu.
Hata hivyo diwani huyo alisema uwepo wa mimea ya
mahindi katika baadhi ya maeneo unachangia wakorea weusi kujificha na kuwavizia
watu wanaopita maeneo hayo.
Post a Comment