Header Ads


IGAD YATAKA MGOGORO WA SUDAN KUSINI UMALIZIKE HARAKA


Jumuiya ya maendeleo Afrika Mashariki na pembe ya Afrika IGAD imeishutumu serikali ya Sudan Kusini kwa kushindwa kukomesha vita ambavyo tayari vimewaua maelfu ya raia nchini humo. Wakati wa mkutano wa siku moja kujaribu kufufua makubaliano ya mkataba wa amani ya mwaka 2015, baraza la mawaziri wa IGAD lilitoa mwito wa kukomeshwa mapigano na kusitisha matumizi ya kijeshi kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wanaoongozwa na Riek Machar.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia aliyeongoza kikao hicho Workneh Gebeyehu amesema hivi sasa wanaandaa kikao cha majadiliano kitakachofanyika mwezi Septemba na kuwa watazungumza na pande tofauti tofauti  zinazoonekana kuhusika na mgogoro huo zikiwemo za serikali  na pande wa upinzani na baadaye kuitisha majadiliano hayo yatakayofanyika mjini Juba.
Mkutano huo ni utekelezaji wa azimio lililopitishwa mwezi uliopita na wakuu wa Jumuiya ya maendeleo Afrika Mashariki na  pembe ya Afrika mjini Adis Ababa ambao walitoa mwito  kwa baraza la mawaziri  wa IGAD kuitisha mkutano kwa ajili ya kufufua na kuweka mkazo katika utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Sudan Kusini.
Südsudan Juba SPLA Rebellen (Getty Images/AFP/S. Bol) Baadhi ya wanajeshi wa SPLA
Taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa mkutano ilisema IGAD inasikitishwa na vurugu zinazoendelea nchini Sudan Kusini, mgogoro wa kibinadamu, kisiasa na kuzorota kwa hali ya uchumi kunakoiathiri nchi hiyo pamoja na maisha ya wananchi wa Sudan Kusini kwa ujumla.
Hatua hii ya IGAD inafuatia kushindwa utekelezaji wa makubaliano ya amani tangu mwaka 2015 kwa ajili ya kurejesha amani nchini Sudan Kusini.
Tayari wachambuzi kadhaa na waangalizi wa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na upinzani ambao walitia saini makubaliano hayo ya amani yaliyoshuhudiwa na kiongozi wa waasi Riek Machar wametangaza makubaliano hayo kufa.
Deng Alor waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini amesema nchi yake ingependelea kuona IGAD ikiendelea kutimiza wajibu wake katika kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo ya amani.
Raia wakabiliwa na hali mbaya
Mgogoro nchini Sudan Kusini umesababisha hali mbaya kwa raia kuliko sehemu nyingine duniani.
Südsudan UN denken über Verstärkung von Unmiss nach (Reuters/A. Ohanesian) Baadhi ya raia nchini Sudan Kusini
Kwa upande mwingine shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International katika ripoti yake mpya linasema  miaka minne ya kipindi cha vita katika taifa hilo changa la  Sudan Kusini  imeshuhudiwa ikukumbwa na vitendo vya  udhalilishaji wa kingono kwa kiwango kikubwa huku maelfu ya wanawake, watoto na baadhi ya wanaume wakiambukizwamaradhi na wengine virusi vya ukimwi.
Ripoti hiyo imekita kutokana na mahojiano waliyofanyiwa wahanga 168 waliofanyiwa udhalilishaji wa kingono nchini Sudan Kusini na katika makambi ya wakimbizi yaliyoko nchi jirani Uganda.
Umoja wa Mataifa mwaka jana uliripoti kuongezeka kwa matukio yanayohusiana na  udhalilishaji kijinsia nchini Sudan Kusini huku asilimia sabini ya wanawake katika makambi ya wakimbizi katika mji mkuu Juba wakibakwa tangu mapigano ya kwa wenyewe nchini humo yalipoibuka Desemba 2013.

                                       Imeandaliwa na Mwandishi: Isaac Gamba/DW

No comments

Powered by Blogger.