HALMASHAURI YA MBEYA KUENDELEZA OPARESHENI YA KUKAMATA MIFUGO
HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imesema oparesheni ya
kukamata mifugo inayozurura hovyo mjini na ufyekaji wa mahindi yaliyopandwa
kwenye maeneo yaliyozuiliwa ni endelevu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la
Mbeya,Patrick Mwakilili alibainisha hayo kwenye mkutano wa hadhara wa mkuu wa
mkoa wa Mbeya Amos Makalla uliofanyika katika kata ya Isyesye jijini hapa.
Mwakilili alisema ukamataji wa mifugo na kufyeka
mahindi haufanyiki kwa maamuzi ya uongozi wa kata ya Isyesye na Itezi kama
inavyotajwa na baadhi ya watu bali ni utekelezaji wa sehemu ya Sheria
ndogondogo zilizotungwa na halmashauri ya jiji.
“Wanaoamua kukamata mifugo siyo diwani wala afisa
mtendaji wa kata.Sheria zinasema hivyo na tutaendelea kusimamia hili.Sawa tu na
kulima mahindi hapa jijini,hatujafyeka kwa kumwonea mtu kama kuna maeneo mnaona
bado yapo mahindi ni kutokana tu na ratiba za kazi lakini sharia ni msumeno
lazima kote oparesheni ifanyike.Hivyo ni vyema mkajua kuwa zoezi hili ni
endelevu”alisisitiza Mwakilili.
Awali Diwani wa kata ya Isyesye Ibrahim Mwampwani
alilalamikia hatua ya wafugaji katika kata yake kukosa usikivu akisema ni mara
kadhaa wamewaonya kwa kukutana nao,kuwaandikia baru na kuwatoza faini
mbalimbali lakini bado wanaacha mifugo yao inazurura.
Mwampwani alisema kutokana na uzururaji wa mifugo
kumekuwa na kazi kubwa ya kutunza miti inayopandwa kwakuwa inaliwa hatua
inayowakatisha tama wananchi walio na mapendi mema na utunzaji wa mazingira.
Alisema wapo wakazi wengi walionuia kupanda miti
kutokana na eneo kubwa la kata ya Isyesye kuwa wazi huku kukiwa na upepo mkali
lakini hofu yao kubwa ni namna ya kuilinda isiliwe na mifugo.
Kwa upande wa oparesheni ya kufyeka mahindi,Diwani
huyo alisema zao hilo limekuwa kichocheo kikubwa cha matukio ya uhalifu ikiwemo
wizi kwakuwa wezi hupata mwanya wa kujificha.
Post a Comment