Header Ads


SERIKALI KATIKA WILAYA YA KYELA YAWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI MAPEMA KWA WANAOISHI MABONDENI


Mkuu wa wilaya ya Kyela BI Cloudia Kitta

KYELA-MBEYA
SERIKALI katika Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya imewataka wananchi wanaoishi katika Meneo ya Mabondeni kuchukua tahadhari ili kuepekana na Athari za Mafuriko zinazoweza kujitokeza kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha.

Mkuu wa Wilaya Kyela, Claudia Kita alilieleza baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo hivi karibuni kuwa kuna uwekano wa kutokea maafa  ya Mafuriko katika Maeneo ya Mabondeni kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Alisema wananchi wanapaswa kuchukua hatua kwa kuhama katika maeneo hatarishi ambayo yanaweza kukumbwa na Mafuriko pamoja na kuzibua Mitaro ili kuruhusu maji kutiririsha maji kwa urahisi.

Kita alisema Wilaya ya Kyela ina Historia ya kukumbwa na Mafuriko mara kwa mara kutokana na hali ya kijiografia ilivyo hivyo inapofika wakati wa msimu wa mvua kila mtu anapasa kuchukua tahadhari ili kujiepusha na madhara ya Mafuriko.



“wakati mwingine maji ya mvua yanaweza yakawa yanatokea katika Wilaya jirani ya Rungwe au Ileje, ninawatake wananchi kuchukua hatua lakini na nyie madiwani mna jukumu la kuhimiza wananchi kuhama katika maeneo hayo, na sisi kama serikali tutahakikisha tunachukua hatua kukabiliana na janga hili,” alisema.

Katika hatua nyingine Kita aliwaonya wananchi wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji pembezoni mwa mito kuacha mara moja kwani imekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira katika Wilaya hiyo.
Alisema sheria inapiga marufuku wananchi kufanya shughuli zozote za binadamu ndani ya mita 60 kutoka kilipo chanzo cha maji na kinyume chake ni kinyume cha sheria za nchi.

Aliwaagiza madiwani kusimamia sheria za Mazingira katika maeneo yao kwani uharibifu umekuwa ukisababisha kina cha maji katika bandari ya Kyela kupungua kwa kasi hali inayotishia meli kushindwa kutia nanga katika bandari hiyo.

Diwani wa kata ya Ikimba Katule Kingamkono alisema wapokea agizo la Mkuu wa Wilaya na kwamba atahakikisha wanalitekeleza kikamilifu ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.

No comments

Powered by Blogger.