WAKUU WA WILAYA ZOTE NCHINI WAAGIZWA KUHAKIKISHA WANAMALIZA TATIZO LA UHABA WA VYUMBA VYA MADARASA
Rukwa
SERIKALI
imewaagiza wakuu wa wilaya zote nchini kuhakikisha wanamaliza tatizo
la uhaba wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wanaofaulu sambamba na kuanza
masomo wasikose nafasi kutokana na uhaba wa madarasa.
Naibu waziri wa Tamisemi Josephat
Kandege ametoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa
halmashauri ya wilaya ya Nkasi ambapo pia aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo
kwa kufanikiwa kujenga vyumba vipya 580 vya madarasa kwa kuwashirikisha
Wananchi.
Amesema hivi sasa kuna wanafunzi
waliomaliza darasa la saba na wanatakiwa kujiunga na masomo ya sekondari mapema
mwakani lakini kuna changamoto kubwa ya nafasi hasa kwa kukosekana kwa vyumba
vya kutosha vya madarasa na kuwa ni lazima kila wilaya ihakikishe inafanya
liwezekanalo kuhakikisha Wanafunzi wote waliofaulu kwenda sekondari wanaendelea
na masomo.
Naibu waziri alisema kuwa katika
taarifa ya wilaya ya Nkasi iliyotolewa na mkuu wa wilaya hiyo Said Mtanda
inaonesha kuwa waliweka mikakati kwa kila kijiji kuhakikisha wanajenga vyumba
vitatu vya madarasa katika mwaka huu na ni mpango ambao ni endelevu kwa kila
mwaka na kuwa kwa kufanya hivyo wilaya imejikuta ikipunguza kwa kiasi kikubwa
tatizo hilo la uhaba wa nafasi za kusomea wanafunzi waliofaulu.
Sambamba na hilo Kandege ameitaka
halmashauri ya Nkasi kuhakikisha inaondoa changamoto zinazowakabili
watumishi hasa za kupanda vyeo kwa wakati ikiwa ni pamoja na stahiki zao ili
kuweza kuwapa mori katika kufanya kazi na kuleta tija.
Awali mkuu wa wilaya ya Nkasi,
Mtanda alimweleza Waziri huyo namna wanavyokabiliana na changamoto mbalimbali
ikiwemo ya vyumba vya madarasa na kumuhakikishia kuwa hakuna mwanafunzi
atashiyendwa kuendelea na masomo kwa sababu ya uhaba wa madarasa na Kuongeza
kuwa wameanza mkakati ifikapo januari mwakani tatizo hilo liwe
limetafutiwa ufumbuzi.
Post a Comment