Header Ads


DIWANI AWATAKA WAZAZI KUTOWAJIA JUU WALIMU PINDI WANAPO WAADHIBU WATOTO wAO

KYELA-MBEYA
DIWANI wa Kata ya Ikimba katika halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Katule Kingamkono amewajia juu  wazazi na Walezi wenye tabia ya kuwafuata shuleni na kuwapiga mkwara walimu wanapowaadhibu watoto wao.
Kingamkono alisema vitendo hivyo vimekuwa vikiwakatisha tamaa walimu katika suala zima la kusimamia nidhamu na Maendeleo ya taaluma ya wanafunzi.
Alibainisha hayo hivi karibuni Wilayani hapa wakati akizungumza kwenye kikao cha wazazi na Walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari Ikimba cha kuhamasisha kuchangia chakula cha Mchana shuleni hapo.
Alisema suala la Kusimamia Nidhamu ya wanafunzi sio la Walimu peke yao bali kila mzazi, mlezi na Jamii kwa ujumla wana jukumu la kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu sambamba na kufuatlia mwenendo wao wa kitaaluma wanapokuwa shuleni na nyumbani.
“Kwa mzazi atakayemfuata mwalimu eti amemuadhibu mtoto wake tutamwita na kumwambia amuhamishe ampeleke kwenye shule nyingine sisi hapa tunataka shule yetu iwe na nidhamu ya hali ya juu,” alisema.
Aidha alisema ili kutokomeza sifuri  katika Matokeo ya Kidato cha nne katika Shule hiyo wazazi na Walezi kwa kushirikiana na uongozi wa katawanapaswa kuchangia chakula.
Kingamkono alisema ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anafanya vizuri kwenye Mtihani wa kidato cha nne hivyo suala la chakula ni Muhimu katika kukuza kiwango cha ufaulu kwenye mitihani yao.
Alisema ameamua kuwashirikisha wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo ili kuangalia njia mwafaka ya kukabilina na changamoto ya utoro na wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao.
Alisema Michango ya chakula itakusanywa na wazazi wenyewe kupitia kamati zao za kuratibu zoezi la chakula na kwamba walimu na ofisi ya Mtendaji wa kata hazitahusika na chochote kwa kuwa suala hilo limeamuliwa na wananchi wenyewe.
 “Tumeona walimu kwa upande wao wanawajibika vizuri na sisi ni lazima tuwaunge mkono angalau kuchangia chakula shuleni, mimi Diwani wenu kwa kuanza nimechangia Gunia tano za Mahindi,lita 20 za mafuta,na Debe tano za maharage nawaombeni mniunge mkono Diwani wenu,” alisema
Mkuu wa shule hiyo Robart Mwakafwila alisema si rahisi wanafunzi ambayo wanakaa na njaa kwa muda mrefu kufanya vizuri katika mitihani yao na kwamba Mpango huo utasaidia kukuza kiwango cha ufaulu katika shule hiyo.
Alisema katika Msimu uliopita jumla ya watahiniwa 66 walimahitimu kidato cha nne ambapo wanafunzi nane ndio waliofeli kwa kupata daraja la sifuri hivyo mikakati yao ni kuhakikisha wanatokomeza kabisa sifuri kwenye mitihani ijayo.
Tumaini Joseph, mkazi wa kata hiyo alisema ikiwa chakula kitatolewa shuleni hapo itasaidia kuongezeka kwa ufaulu kwa kuwa wanafunzi utaotokana na kuongezeka kwa jitihada za kujisomea.

No comments

Powered by Blogger.