MGODI WA KIWIRA KUFUFULIWA TENA
NAIBU Waziri wa Madini,Dotto Biteko amewataka wakazi
wa vijiji vilivyopo jirani na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira wilayani hapa
kuwa watulivu na kuwahakikishia kuwa mgodi huo utafufuliwa na watapata ajira
kama zamani.
Biteko alisema hayo katika nyakati tofauti alipokuwa
wilayani Kyela na Ileje baada ya kutembelea mradi huo na kujionea uwekezaji
uliofanyika wakati mgodi huo ulipokuwa ukifanya kazi.
Miongoni mwa maeneo ambayo naibu waziri huyo
alilazimika kuzungumzia mikakati ya Serikali ni pamoja na alipokutana na wakazi
wa vijiji jirani walioomba kujua hatima ya mgodi huo sambamba na maslahi ya
waliokuwa wafanyakazi wakati ulipokuwa ukifanya kazi aliokutana nao wakati
akitoka mgodini hapo.
Wananchi hao waliokusanyika getini waliomba Serikali
kuufufua mgodi huo wakisema kutofanya kazi kwa mgodi huo kumewasababishia kuwa
na hali ngumu ya kimaisha ambapo baadhi yao wamelazimika kujiingiza katika
ujangili wa uchomaji mkaa hatua inayohatarisha misitu ya asili.
Hata hivyo naibu Waziri alisema nia ya Serikali ni
kufufua mradi huo hivyo wakazi wa maeneo ya jirani hawana budi kuwa watulivu
wakati jitihada mbalimbali zikifanyika.
Aidha Biteko aliagiza uongozi wa mgodi uliopo hivi
sasa kutoaa kipaumbele kwa wakazi wa maeneo ya jirani kwa kuwapa ajira za muda
zikiwemo za kufanya usafi ndani ya mgodi huo pale Serikali inapotoa fedha ili
wazidi kushiriki katika kulinda mali za umma zilizopo kwenye eneo hilo wakati
jitihada za kufufua mgodi zikiendelea kufanyika.
“Tunapenda mtambue kuwa huu ni moja kati ya migodi
mikubwa ambayo Serikali kamwe jhaiwezi kuiacha ikafa.Kuweni na subra kama
ambavyo mmekuwa watulivu kwa muda mrefu.Tuna wahakikishia hakuna aliye na haki
taachwa asilipwe hapa.Na tunawahakikishi mgodi huu lazima ufufuliwe.Tungekuwa
hatuna nia ya kuufufua tusingekuwa na sababu ya kuharibu mafuta ya Serikali
kuja huku”
“Lakini pia nimeagiza uongozi,Serikali inaleta fedha
hapa kwaajili ya shughuli ndogondogo wakati tukiendelea kufanya jitihada za
kufufua mgodi.Hizi kazi wawape ninyi miliopo jirani ili walau kasungura haka
kadogo na ninyi mkafaidi wakati tunaendelea na mambo mengine.Sasa sasa hata
hiki kidogo tunacholeta nacho msipate,itakuwa si haki na Serikali yetu haitaki
hivyo.”alisisitiza Biteko.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kyela,Claudia Kita
na mkuu wa wilaya ya Ileje Joseph Mkude walisema wakazi wa wilaya hizo mbili
wana uchu wa kuona mgodi huo unafufuliwa na kuanza kufanya kazi ili waweze
kunufaika nao kama ilivyokuwa awali.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela,Dk
Hunter Mwakifuna alisema kufufuliwa kwa mgodi huo kutapunguza changamoto ya
uhaba wa ajira uliopo katika wilaya hizo mbili na kuwa Serikali nayo itanufaika
kwa kiasi kikubwa hasa kutokana na uwepo wa Meli kubwa mpya katika ziwa Nyasa
zitakazotumika kusafirisha makaa yam awe kwende nchi jirani.
Post a Comment