MKANDARASI KUFIKISHWA MAHAKAMANI
SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini(TAA)
kuipeleka mahakamani kampuni ya DB Shapraya kwa kushindwa kutekeleza kwa wakati
kazi ya ujenzi wa Jengo la Abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe
uliopo mkoani Mbeya.
Serikali pia imeagiza TAA kuanza kukata fedha kama
adhabu ya kuchelewesha mradi kuanzia Januari 30 mwaka huu kwa kampuni hiyo
ambayo licha ya kulipwa fedha zote na Serikali imeshindwa kutekeleza mradi huo.
Naibu waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano,Mhandisi
Atashasta Nditiye alitoa maagizo hayo juzi(jumamosi) alipofanya ziara ya
kushitukiza katika uwanja wa Songwe na kukuta hakuna kazi yoyote inayoendelea.
Nditiye alisema ni jambo lisilokubalika kuona fedha
ya watanzania iliyolipwa ikiendelea kuchezewa kwa miaka mitano huku kazi
iliyotarajiwa kufanyika ikiendelea kupigwa danadana.
“Mkataba ulielekeza kwamba hili jengo liishe ndani
ya miezi minane.Kulitokea matatizo ya hapa na pale,kubalilisha design na design
ikabadilishwa kweli kukawa na delay ya mabadiliko na ilikubalika kwa pande zote
mbili.Lakini vile vile kukawa na tatizo la kifedha kutoka Serikalini sababu
zikatolewa mkandarasi akazielewa na Serikali ikazielewa.”
“Ikafika mahali 2015 mapema mwezi wa pili pesa flani
ya ajabu ajabu ikatoka kwaajili ya kumpatika mkandarasi ajenge amalizie hili
jengo lakini tangu kipindi hicho apate hiyo pesa kwanza yeye mwenyewe alikuwa
haamini ameipataje pataje!Kwa maneno yao lakini wao wanajua waliipataje kwa
sababu kwa bahati mbaya au nzuri kuna ujanja ujanja mwingi sana ulikuwa
unatumika hapa siku za nyuma”
“Lakini mpaka saa hizi ninavyoongea ni kwamba hawa
watu hawaidai Serikali fedha yoyote .Sasa hivi Serikali ndiyo inawadai kwa hatua
iliyofikiwa.Nawashauri waache kufanya kazi kiujanja ujanja na nitataka TAA
kuanzia tarehe 31 ambayo ni deadline waliyopewa na waziri waanze kukata hasara
inayotokana na kuchelewesha kazi” alisisitiza naibu waziri
Alisema kwa hali aliyoiona baada ya kutembelea mradi
huo mkandarasi huyo hata angeongezewa muda zaidi mwaka huu ungemalizika pia
pasipo jengo hilo kukamilika na hata mwakani pia hivyo hakuna sababu ya
kuendelea na kazi hiyo.
“Nimeingia hapa hakuna shughuli yoyote inayoendelea
ninyi wenyewe mmeona. Tulichofanikiwa ni kuvalishwa haya manguo na kupewa
makofia lakini hakuna kazi,sehemu yenye kazi ninyi wenyewe mnajua inavyokuwa
imechangamka.Hakuna mafundi tumekuta hawa wasimamizi tu ambao nao ni wageni
hata hawajui lolote wana miezi mitatu”
“Nimemuona mkandarasi mshauri naye yuko hapa naye
amekuja kwakuwa amejua nakuja hana maelezo yoyote kwa ujumla.Ataniambia nini
wakati mkandarasi hayupo kwenye site.Taa wajiandae kumpeleka mahakamani”
Nditiye alisema lengo la Serikali ni kuona miradi
inayotakiwa na wananchi inafanyika na kumalizika kwa wakati,hivyo kwa mradi huo
atatafutwa mkandarasi mwingine tatakayemalizia ujenzi huo ndani ya mwaka huu.
“Tunataka awamu hii kuonyesha kwa vitendo kuwa
tunafanya kazi za wananchi.Na tumejipanga kweli kufanya kazi za nchi.Mh Rais
halali anatafuta pesa,pesa inalipwa mtu hataki kufanya kazi anakimbia
site.Tutahakikisha hizi pesa anazitema na kweli tutahakikisha zinarudi hizi
pesa na hili jengo litaisha kwa wakati tunaohitaji sisi”
Naibu waziri huyo alilaumu hatua ya baadhi ya wakandarasi
wazawa kutowajibika kwa kazi wanazopewa licha ya Serikali kuwapa upendeleo
ikiamini fedha izaowalipa zitabakia hapa nchini na kuwaongezea mitaji
watanzania.
Alisema hatua stahiki dhidi ya mkandarasi huyo
haitoishi kumfikisha mahakamani na kumtoza adhabu ya fidia ya kuchelewesha
mradi bali pia kumshitaki katika bodi ya makandarasi nchini ili nayo ichukue
hatua stahiki.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa viwanja vya ndege
vya mikoa,Joseph Nyahende alisema mradi huo ulikuwa wa kukamilisha kazi tatu
ambazo ni ujenzi wa maegesho ya ndege,barabara na jengo la abiria.
Alisema ulikuwa ni mkataba wa shilingi bilioni 11 na
hadi Desemba mwaka jana Bilioni 9.7 zilikuwa zimelipwa kwa mkandarasi hivyo kwa
hatua ya kazi iliyofikiwa mkandarasi huyo haidai Serikali bali anadaiwa kazi.
Kwa upande wake Mkandarasi mshauuri kutoka kampuni
ya Unitec ya nchini Dubai,Mhandisi
Silanda Dustan alisema kinachoonekana ni mkandarasi kushindwa kutekeleza
majukumu ya kazi aliyopewa wakati wananchi wanamatumaini na wanasubiri
miundombinu ili wakuze uchumi wao.
“Sisi tumeshauri Serikali kuwa mkandarasi hawezi
tena kufanya kazi hii hivyo ni wakati kuchukua hatua zinazostahiki.Hayupo
kazini.Kuna hiyo hasara ya kuchelewa kwa mradi.Kama abiria wangekuwa wanapita
hapa Serikali ingepata kodi na pesa ya wananchi iliyotolewa kwaajili ya ujenzi
huu ingekuwa imeanza kurudi sasa”
Post a Comment