RAIS MAGUFULI ATOA MILIONI 10 KWA WANANCHI WA HANDENI
Rais
John Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kuwapatia Sh milioni 10
wananchi wa kijiji cha Kwamkonga wilayani Handeni, mkoani Tanga
walizoomba Agosti 3 mwaka jana.
Waliomba fedha hizo kwa ajili ya kuboreshewa huduma za afya katika zahanati ya kijiji hicho iliyokuwa na uhaba wa vifaa tiba.
Rais
Magufuli alipita katika kijiji hicho kilichopo pembezoni mwa barabara
ya Chalinze-Segera na kuzungumza na wananchi hao wakati akielekea mjini
Tanga kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka
Chongoleani mkoani Tanga hadi Hoima nchini Uganda.
Wananchi
hao walimweleza Rais matatizo mbalimbali inayoikabli zahanati yao hasa
suala la maabara ambayo walikuwa wakikosa huduma hizo hadi wazifuate
katika kituo cha afya Mkata au kwenda katika hospitali ya wilaya
Handeni.
Akikabidhi
kwa niaba ya Rais, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema Rais
alipopewa malalamiko na wananchi kuhusu kuboreshwa zahanati hiyo,
ameleta kiasi cha milioni 10 ambacho kimetumika kununua vifaa mbalimbali
vinavyopaswa kuwekwa kwenye maabara.
Shigela
alisema Rais anajali wananchi wake waliomchagua ndiyo maana ameweza
kuleta fedha hizo ili wapatae huduma karibu na vijiji vyao kwa lengo la
kupunguza safari za kwenda umbali mrefu kufuata huduma za maabara.
Mganga
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Dk Credianus Mgimba alisema walipopokea
fedha hizo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga, waliziweka
katika akiba ya zahanati ya kijiji hicho ambapo walifanya manunuzi ya
vifaa hivyo.
Akitoa
shukrani Mkuu wa wilaya hiyo, Godwin Gondwe alimshukuru Rais kwa
kutekeleza ahadi hiyo ambayo itawawezesha wananchi wa kijiji hicho na
vijiji jirani kupata huduma bora za afya hasa za maabara na kupunguza
msongamano katika vituo vya afya na hospitali ya wilaya.
Post a Comment