MATOKEA YA UCHUNGUZI KUHUSU KAULI YA ASKOFU ZACHARY KAKOBE
Kufuatia
kauliiliyotolewa na Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la Full Gospel
Bible Fellowship katika mahubiri ya Ibada ambayo alisema kuwa “Yeye ana
pesa kuliko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ilifanya uchunguzi ili kubaini usahihi wa kauli
hiyo.
Yafuatayo ni mambo ambayo yalibainika baada ya kufanyika uchunguzi kuhusu kauli ya Askofu Zachary Kakobe;
1.Askofu
Zachary Kakobe hana akaunti wala fedha katika taasisi yoyote ya fedha
hapa nchini. Aidha uchunguzi ulibaini kuwa Askofu Kakobe ni mmoja wa
wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa (signatories) zilizopo katika
benki ya NBC zenye jumla ya kiasi cha shilingi 8,132,100,819.00, kiasi
hiki cha fedha kimetokana na sadaka, zaka na changizo ambazo zinatolewa
na waumini wa kanisa tajwa hapo juu, hivyo kwa mujibu wa Sheria
hakitozwi kodi.
2.Kanisa
lilikwepa kulipa kodi kiasi cha shilingi 20,834,843.00 ambazo
zilitokana na uwekezaji katika makampuni ya kukuza mitaji.Kodi hiyo
imelipwa baada ya uchunguzi.
3.Kampuni
inayomilikiwa na watoto wa Askofu Zachary Kakobe ilikwepa kulipa kodi
kiasi cha shilingi 37,280,030.00 ambazo zimelipwa baada ya uchunguzi.
Kwa ujumla, kiasi cha kodi kilicholipwa kutokana na uchunguzi huu ni
shilingi 58,114,873.00.
4.
Kanisa linatunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo na ‘majaba’
kinyume na taratibu za utunzaji wa fedha, lakini pia uwekaji na utoaji
wa fedha nyingi kutoka benki haushirikishi vyombo vya ulinzi na usalama
kwa ajili ya usalama wa fedha zenyewe na wahusika.
5.Pia
ilibainika kwamba Kanisa halitengenezi hesabu za Mapato na Matumizi ya
Fedha kitu ambacho ni kinyume na Katiba ya Kanisa pamoja na sheria za
usimamizi wafedha ambayo imepelekea matumizi mabaya ya fedha za waumini
kama vile safari za nje ya nchi ambazo zimedhaminiwa na Kanisa lakini
wanaosafiri ni Askofu na familia yake. Vile vile fedha za Kanisa
zinatumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu, kwa jina lake na wala si kwa
jina la Kanisa, kitu ambacho ni kinyume na taratibu za Kanisa.
Aidha,
wakati uchunguzi huo ukiendelea,mnamo tarehe 24.01.2018 Askofu Kakobe
aliandika barua kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuomba radhi kutokana na kauli yake ya kebehi pamoja na matamshi yake ya
dharau kwamba ana pesa nyingi kuliko Serikali.
WITO:
•
Mamlaka ya Mapato Tanzaniainatoa wito kwa Taasisi zote za dini ambazo
zinajihusisha na shughuli zozote za kiuchumi kulipa kodi stahiki na kwa
wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi.
•
Mamlaka ya Mapato Tanzania inazitaka Taasisi zote za kidini kufuata
katiba zao ikiwa ni pamoja na kutengeneza hesabu za mapato na matumizi.
Charles E. Kichere
KAMISHNA MKUU
MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Post a Comment