Header Ads


CHAMA CHA MAPINDUZI MKOANI MBEYA KUFANYA MAHADHIMISHO YA MIAKA 41



MBEYA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kinatarajia kuadhimisha miaka 41 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo Usafi na misaada kwa watoto yatima.

Akizungumza katika warsha ya Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbeya mjini iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Wilson Nkambako alisema sherehe hizo zitaanza Februari 3 na kuhitimishwa Februari 5, mwaka huu.

Nkambako alisema maadhimisho hayo yatafanyika kimkoa katika Kata ya Itezi ambapo Februari 3, mwaka huu itafanyika semina elekezi kwa Mabalozi wote wanaotokana na Chama cha Mapinduzi kutoka Kata za Itezi, Igawilo, Uyole na Nsalaga.

Alisema siku ya Pili yaani Februari 4, mwaka huu Chama kitafanya usafi katika kituo cha Afya Igawilo, Zahanati ya Nsalaga na Uyole kisha kutembelea kituo cha Watoto Yatima Nsalaga na kutoa msaada.

Aliongeza kuwa siku ya kilele yaani Februari 5, mwaka huu Chama Mkoa kitahitimisha sherhe zake kwa kufanya mkutano katika soko jipya lililopo Gombe kusini Kata ya Itezi jijini Mbeya.

Katika hatua nyingine Nkambako alisema Chama kimepokea maagizo kutoka makao makuu kikiagiza kila Tawi, Kata, Wilaya hadi Mkoa kufungua akaunti katika benki ya Posta(TPB).

Alisema lengo la akaunti hizo ni katika kudhibiti mali za Chama kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya kufungua akaunti mbili moja ikiwa ya makusanyo na nyingine ya matumizi.

Alisema katika ngazi ya Kata na Matawi wao wanafungua akaunti moja ya matumizi pekee kwa akaunti ya makusanyo itatumika ambayo imefunguliwa na Wilaya.

Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya mjini, Gerald Mwadalu alisema katika kufanikisha maadhimisho hayo imeundwa kamati maalumu ya kushughulikia maandalizi yake.

Alisema mbali na sherehe hizo kufanyika kimkoa katika Kanda ya Uyole, Kanda zingine zitaadhimisha sherehe hizo kwa kufanya shughuli za kijamii katika maeneo yao huku wakiongozwa na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya.

Aliongeza kuwa katika sherehe hizo ni katika kuonesha uhai wa Chama na imani kwa Wakazi wa Jiji la Mbeya kuwa Chama cha Mapinduzi kipo na kimedhamiria kulikomboa Jimbo kutoka upinzani pamoja na serikali za Mitaa.

No comments

Powered by Blogger.