TAASISI YA HAKI ZA BINADAMU NA WADAU WA HABARI NCHINI WAMEUNGANAKULAANI KITENDO CHA WAZIRI WA HABARI,TAMADUNI,SANAA NA MICHEZO DR.HARISON MWAKYEMBE KULIFUNGIA GAZETI LA MAWIO
DAR ES SALAAM
Jana, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki zaBinadamu (THDRC) na Umoja wa Klabu za Habari Tanzania (UTPC) kwa pamoja.
waliungana na kueleza kuwa sheria iliyotumika kulifungia gazeti hilo
ilipaswa kutumiwa na Mahakama kutoa adhabu hiyo.
Mratibu wa THDRC, Onesmo Olengurumwa alipinga utaratibu wa kisheria wa
kumpa waziri mamlaka makubwa katika sekta ya habari huku sheria
iliyopita na ya sasa zikiwa hazina tofauti yoyote hasa katika mamlaka ya
waziri kuamua kulifungia gazeti kwa makosa atakayoona yeye kuwa ni
kinyume na masilahi ya umma.
“Sheria hii mpya imeendelea kumfanya waziri awe mhariri mkuu,
mlalamikaji, mpelelezi, mwendesha mashtaka na hakimu kwa wakati mmoja,”
alisema.
Kifungu cha 59 namba 12 cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016
ndicho kilichotumiwa na waziri kulifungia gazeti la Mawio kwa miaka
miwili kuanzia Juni 15 ikiwa ni mara ya pili tangu Serikali kulifutia
usajili gazeti hilo Januari 2016 kabla ya kushinda mahakamani.
Olengurumwa alisema kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania
Watanzania wana uhuru wa kutoa maoni na kuchapisha habari kuhusiana na
mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao.
“Kitendo cha kuzuia Watanzania au vyombo vya habari visichapishe picha
za viongozi wastaafu hasa katika mijadala ya kitaifa ni kuwaziba midomo
katika sakata la vita dhidi ya wizi wa madini nchini,” alisema.
Kuhusu kifungu kilichotumika kutoa adhabu kwa gazeti hilo alisema,
“Ikumbukwe kwamba mamlaka yenye uwezo wa kutoa haki katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni Mahakama pekee kwa mujibu wa ibara ya 107 (A)
(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Aliongeza kuwa kifungu kilichotumika kutolea adhabu hakielezi kosa
lililotendwa na gazeti na kisheria, adhabu haitolewi bila kuwapo kwa kosa.
Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo alisema kitendo kilichofanyika ni
kumnyima haki mwandishi kutoa maoni. Alisema mbali na taaluma yake, bado
ni Mtanzania mwenye haki ya kujieleza na kutoa mawazo yake ambayo
yanalenga masilahi ya nchi kama ilivyo katika makala iliyochapishwa
katika ukurasa wa 12 wa gazeti la Mawio.
“Tumebaini hakukuwa na mawasiliano na utaratibu mzuri wa kuwasikiliza
viongozi wa Mawio kwani idara ya habari iliwasiliana kwa njia isiyo
rasmi na Mhariri wa Mawio bila ya kutoa barua yoyote kiofisi, pamoja na
kwamba hakukuwa na mawasiliano ya kiofisi zaidi ya simu, Mawio
waliandika barua ya kueleza sababu za kuchapisha gazeti lao na taarifa
husika,” alisema Nsokolo.
Kaimu Katibu Mtendaji wa MCT, Pili Mtambalike aliiomba Serikali itengue
uamuzi wake wa kulifungia gazeti hilo kwa kuwa ni kinyume na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Huduma ya Habari ya
mwaka 2016 ambayo kimsingi haimpi mamlaka waziri kutoa adhabu hiyo.
Alisema katika kutimiza nia ya Rais ya kukabiliana na watuhumiwa wote wa
kashfa ya madini, yampasa kuruhusu wananchi kuwajadili kwa uhuru wale
wote waliotuhumiwa kuhusika bila kujali kwamba wametajwa katika taarifa
ya kamati au la.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dk Hassan Abbasi
alisema jana kuwa kabla ya kutoa matamko yoyote, wanaharakati hao
wanatakiwa kusoma sheria.
“Ukisoma katika mkataba wa kimataifa wa haki za kisiasa na za kiraia wa
1966, umeaninisha mambo manne ambayo ni kutoingilia faragha ya mtu,
hadhi, staha, usalama wa taifa, afya ya umma na amani ya nchi,” alisema.
Alisema katika ibara ya 30 na 18 ya Katiba vipengele hivyo vimeanishwa
na kusema wanaharakati hawawasaidii wanahabari, bali wanaangalia hatua
zilizochukuliwa na Serikali bila kuzingatia makosa yaliyofanywa na
wanahabari au vyombo vya habari.
“Serikali itakuwa mlezi wa kuwapongeza waandishi wanaofuata maadili ya
habari na haitasita kuchukua kwa wanaokiuka maadili.
“Wasiingize hisia katika sheria, wajue kuwa nguvu aliyopewa waziri ni ya
kisheria kama zilivyo taasisi nyingine na nimewasikia wanaenda
mahakamani, tutakutana nao huko,” alisema Abbas.
Mhariri Mtendaji wa Mawio, Simon Mkina alikaririwa na Shirika la Habari
la AFP akisema wanatafuta wakili mzuri na watafungua kesi kupinga
kufungiwa huko wiki hii.
Pia alisema tangu gazeti hilo lifungiwe amekuwa akipokea simu za vitisho.
“Baada ya gazeti kufungiwa, nimepokea simu tatu za vitisho. Simu
mojawapo ambayo ilikuwa ni sauti ya kiume, iliniuliza kama maisha yangu
yana thamani na simu yenyewe haikuonyesha namba, sikuweza kuipiga tena,”
alisema.
Post a Comment