ASKOFU MWINGINE WA KANISA LA ANGLIKANA ASHITAKIWA
DAR ES SALAAM
Ikiwa imepita takriban miezi sita tangu aliyekuwa Askofu wa Kanisa la
Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa avuliwe
madaraka na uongozi wa juu wa kanisa hilo, Baraza la Wazee wa Nyumba ya
Walei wa Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), limeshtaki Askofu wao,
Boniphace Kwangu.
Dk Mokiwa ambaye alishtakiwa na kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali dhidi
ya kanisa hilo, alivuliwa madaraka na Askofu Mkuu, Jacob Chimeledya.
Katika mashtaka yake, baraza la walei la DVN limemuomba Askofu
Chimeledya kutatua mgogoro baina ya waumini na askofu huyo uliodumu kwa
miaka minne sasa.
Alipotafutwa kwa simu, askofu huyo alisema kwa kifupi kuwa, “Kuongea na
mwandishi wa habari ni kupoteza muda wangu kama hayo yapo upo
utaratibu.” Baada ya kauli hiyo alikata simu.
Akitoa tamko la wazee hao jana katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa
Kuu la Mtakatifu Nicholaus jijini Mwanza yalipo makao makuu ya dayosisi
hiyo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Osoro Nyawanga alisema askofu huyo
ameligawanya kanisa katika makundi.
Alisema hawajapata huduma za kiaskofu kwa kipindi cha miaka miwili,
ikiwa ni pamoja na watoto kutopata kipaimara.
Nyawanga alisema licha ya viongozi wa kanisa hilo kulipigia kelele suala
hilo kwa nyakati tofauti bado linazidi kushamiri.
Alisema Askofu Kwangu anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali za kanisa na
kuwafukuza wachungaji huku akiwaweka anaowajua yeye na kwa miaka miwili
sasa hajakalia kiti chake.
“Kuna fedha Sh190 milioni za International School iliyopo Isamilo jijini
Mwanza, mali ya kanisa zimetafunwa na shule huenda itafungwa kwa sababu
ina hali mbaya kwa sasa. Askofu hatumtaki tunapaza sauti askofu mkuu aje
atumalizie mgogoro huu haraka, kanisa linaangamia na maendeleo
yamekwama,” alisema Nyawanga
Muumini wa kanisa hilo, Peter Mlashani alisema mgogoro huo umekwamisha
huduma nyingi za kanisa na kuwaathiri.
Joyce Abisai alisema, “Kweli kanisa linapoelekea ni pabaya hata nje ya
kanisa tunakuwa na mwonekano na taswira mbaya.”
Post a Comment