BARABARA YA UYOVU-BWANGA-BIHARAMULO KUKAMILIKA MWISHONI MWA MWAKA
BIHARAMULO
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa KM 112 inayojengwa na mkandarasi wa Kampuni ya Synohydro Corporation itakamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Prof. Mbarawa amezungumza hayo mkoani Kagera, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kumtaka mkandarasi aongeze kasi ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
“Hakikisheni mnaongeza kasi ya ujenzi ili muweze kukamilisha ujenzi huu kwa wakati iwezekanavyo”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amemsisitiza mkandarasi kuzingatia viwango vilivyopo katika mkataba kwani mwisho wa siku lazima watanzania wapate barabara inayokidhi mahitaji yao na ubora wake.
Amewapongeza wasimamizi wa barabara hiyo ambao ni kutoka kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kupitia kitengo chake maalum cha wahandisi washauri wazawa (TECU), kwa kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi M/S Sinohydro Corporation kwa ukaribu.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Geita Eng. Harun Senkuku amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa changamoto ya fidia iliyokuwa inawakabili sasa imemalizika na kiasi cha shilingi milioni 700 zimetumika kukamilisha ulipaji fidia kwa wakazi wote.
Amemhakikishia Waziri kuwa TANROADS itaendelea kumsimamia mkandarasi huyo ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha ya Serikali inapatikana.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo KM 112 umehusisha ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa KM 45 na barabara ya Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa KM 67.
Post a Comment