KESI YA KABURU, AVEVA YAPIGWA KALENDA TENA HADI SEPTEMBA 8
Kesi inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ leo imeendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo upande
wa mashtaka umeieleza mahakama hiyo kwamba umekusanya nyaraka za upelelezi na zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi hivyo hivyo wanasubiri ripoti.
Hayo yamesemwa na Wakili wa Serikali, Estazia Willson mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa ambapo aliiiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Septemba 8 mwaka huu.
Aidha, hakimu aliutaka upande wa mashtaka kuharakisha ripoti hiyo ya uchunguzi akisema kwamba watuhumiwa wako rumande hivyo si bora kesi hiyo kuahirishwa kila mara.
Wawili hao leo walipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam kwa mara ya saba tangu Takukuru ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) iwatie hatiani na kusomewa tena mashitaka hayo kabla ya Hakimu Victoria Nongwa kuiahirisha tena kesi hiyo hadi Agosti 16, mwaka huu.
Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.
Kwa sasa nafasi zao zinakaimiwa na Salim Abdallah ‘Try Again’ katika Urais na Iddi Kajuna katika Makamu wa Rais, ambao wamejitahidi kuiongoza vizuri klabu tangu wenzao wapate matatizo hayo.
Post a Comment