BEKI AGGREY NA SURE BOY WAONGEZA MIKATABA AZAM FC
Nyota wawili wa Azam FC, nahodha msaidizi Aggrey Morris na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ jana Jumanne waliongeza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Zoezi la kuingia mikataba hiyo lilisimamiwa na Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Abdulkarim Mohamed ‘Popat’, kwenye Ofisi za timu hiyo Mzizima, zilizopo Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Awali mikataba yao ilitarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu huu, hivyo kwa kuongeza mikataba mipya, itawafanya wachezaji hao kusalia ndani ya viunga vya Azam Complex hadi mwaka 2019.
Uongozi wa Azam FC kwa kushirikiana na benchi la ufundi umewaongeza mikataba mipya wachezaji hao, kutokana na viwango vyao bora na mchango mkubwa wanaoendelea kuutoa ndani ya kikosi hicho.
Wawili hao ni wachezaji wakongwe ndani ya kikosi hicho, Sure Boy akianzia kuichezea Azam FC tokea timu hiyo ilipokuwa madaraja ya chini kabla ya kupanda nayo Ligi Kuu mwaka 2008 huku Moris akijiunga na mabingwa hao mwaka 2009 akitokea Mafunzo ya Zanzibar.
Post a Comment