TETESI ZA USAJILI LEO SIKU YA JUMAPILI YA TAREHE 17.6.2017
Machesha blogspot inakuletea muhtasari wa tetesi na habari za uhamisho kutoka Ligi Kuu Uingereza, La Liga, Serie A, Bundesliga na kwingineko
UTD YATAKIWA KUTOA £50M KUMSAJILI DIER
Manchester United wameambiwa watoe paundi milioni 50 au zaidi kumsajili kiungo wa Tottenham Eric Dier, Telegraph limeripoti.
Jose Mourinho anataka mchezaji huyo wa Spurs asajiliwe kabla ya msimu mpya kuanza, lengo ni kutafuta mrithi wa kudumu wa Michael Carrick.
MENDES AIAMBIA REAL RONALDO ANA OFA KUTOKA UINGEREZA
Wakala wa Cristiano Ronaldo, Jorge Mendes ameiambia Real Madrid kuwa mshambuliaji huyo amepokea ofa kadhaa kutoka klabu za Ligi ya Uingereza, kwa mujibu wa Cope .
MAN UTD & JUVE ZAMFUATILIA GOMES
Manchester United na Juventus zinafuatilia maendeleo ya kiungo wa Barcelona Andre Gomes, kwa mujibu wa habari za AS .
Gomes amekuwa na mwanzo mgumu Barcelona na Mreno huyo anaweza kutimkia kwenye klabu mojawapo kati ya Juventus na Manchester United.
RONALDO KUGHARIMU €400M
Klabu yoyote inayotaka kumsajili Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid italazimika kutoa kwa mkupuo mmoja euro milioni 400, kwa mujibu wa Gazzetta dello Sport .
Kiasi hicho ni ada ya uhamisho pamoja na ujira wake, na habari kutoka Ureno zinadai mshindi huyo wa Ballon d'Or anataka kuondoka Hispania majira ya joto.
BAKAYOKO AAMUA KUTUA CHELSEA
Kiungo wa Monaco, Tiemoue Bakayoko amechagua kujiunga na Chelsea badala ya Manchester City na Man United, kwa mujibu wa L'Equipe, kupitia Sport Witness .
RONALDO ANATAKA KUONDOKA MADRID
Cristiano Ronaldo amemwambia rais wa Real Madrid, Florentino Perez kuwa anataka kuondoka klabuni hapo majira ya joto, kwa mujibu wa A Bola .
Mreno huyo alitajwa katika shutuma za kukwepa kodi, na amefanya maamuzi yasiyoweza kupinduliwa.
BAYERN BADO WANAMTAKA VERRATTI
Bayern Munich bado wanataka kumsajili Marco Verratti kutoka PSG licha ya kumpata Corentin Tolisso kutoka Lyon, limeripoti Bild .
PEP ANAMTAKA KROOS CITY
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola ameshaanza mazungumzo katika harakati za kumsajili kiungo wa Real Madrid Toni Kroos, kwa mujibu wa Don Balon .
CONTE KUONDOKA CHELSEA?
Meneja wa Chelsea Antonio Conte amekerwa na klabu hiyo kutokubali kufanya usajili dirisha la uhamisho wa majira ya joto na anaweza kuondoka klabuni hapo kwa mujibu wa Sky Sport Italia .
Conte, ambaye aliondoka Juventus kwa sababu ya mazingira kama hayo, anataka wachezaji maalumu kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini anaona miamba hao wa London hawana mpango wa kuingia sokoni.
Bosi wa zamani wa Borussia Dortmund ametajwa kuwa mrithi wake.
REAL YAIZIDI PSG KUMFUKUZIA DONNARUMMA
Real Madrid wanaongoza katika mbio za kumsaini Gianluigi Donnarumma kutoka AC Milan, lakini wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa Paris Saint-Germain, kwa mujibu wa Sky Sport Italia .
MADRID WANATAKA £78M KWA AJILI YA MORATA
Real Madrid wametangaza kuwa bei ya Alvaro Morata ni paundi milioni 78 ikiwa Manchester United wanataka kweli kumsajili mshambuliaji huyo, kwa mujibu wa The Independent .
United walikuwa wakitarajia watafanikiwa kumsajili mchezaji huyo kwa kiasi cha paundi milioni 60, lakini rais wa klabu Florentino Perez amesema kwa bei hiyo mchezaji huyo hatoki.
JUVE WAKATAA OFA YA ARSENAL KWA CUADRADO
Dau la Arsenal la paundi milioni 17 kwa ajili ya winga wa Juventus Juan Cuadrado limekataliwa na mabingwa hao wa Serie A, kwa mujibu wa The Sun .
Arsene Wenger anataka kujiandaa kwa maisha bila ya Alexis Sanchez kwenye kikosi chake na anaamini Cuadrado angeziba vema pengo la mchezaji huyo anayetaka kuondoka Emirates.
Juventus wamesisitiza kuwa bila ya ofa ya paundi milioni 30 hawawezi kushawishika kumuuza mchezaji wao.
TIMU ZA LONDON ZAMWANIA KOVACIC
Arsenal na Tottenham zinapigana vikumbo kuiwania saini ya mchezaji wa Real Madrid Mateo Kovacic, kwa mujibu wa Diario Gol .
Hakuna hata moja kati ya klabu hizo iliyotoa ofa kwa ajili ya mchezaji huyo raia wa Croatia, AC Milan na Inter zinatamani huduma ya mchezaji huyo pia.
ARSENAL YAMTENGEA DAU KJAER
Arsenal imetoa dau la euro milioni 12 kwa ajili ya mchezaji wa Fenerbahce Simon Kjaer, kwa mujibu wa TurksVoetbal .
Miamba hao wa Emirates watakabiliwa na ushindani kutoka kwa AC Milan ingawa klabu hiyo ya Uturuki haipo tayari kupokea fedha chini ya €15m.
FENERBAHCE YAMFUKUZIA VARDY
Fenerbahce wanajiandaa kumsajili mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy, kwa mujibu wa DHA .
Miamba hao wa Uturuki wanatafuta mrithi wa Robin van Persie na pia wanataka kumsajili Ahmed Musa kutoka timu moja na Vardy.
ARSENAL YAMFUKUZIA SMALLING
Arsenal ni miongoni mwa klabu zinazofuatilia maendeleo ya beki wa Manchester United, Chris Smalling kwa mujibu wa The Sun .
Mashetani Wekundu wakiwa katika harakati za kumsajili Victor Lindelof, wanaweza kumwachilia Muingereza huyo majira ya joto, West Ham nao wanataka kumsajili.
JUVE YAMFUKUZIA MAHREZ
Juventus ni klabu nyingine ya Ulaya inayotaka kumsajili winga wa Leicester City Riyad Mahrez, kwa mujibu wa Daily Mirror .
Arsenal wamehusishwa na tetesi za kutaka kumsajili Mwalgeria huyo, Barcelona nayo ikiaminika kuwa moja ya timu anazoweza kujiunga nazo.
MAN UTD WANAMTAKA MATIC, SIYO FABINHO
Jose Mourinho hamtaki Fabinho wa Monaco, badala yake anataka kumsajili Nemanja Matic kutoka Chelsea, kwa mujibu wa Manchester Evening News .
CHELSEA WANAMTAKA CABALLERO
Chelsea wanataka kumsajili kipa wa zamani wa Manchester City Willy Caballero kushirikiana na Thibaut Courtois, Mwandishi wa Argentina Cesar Luis Merlo amekiambia TyC Sports .
Caballero amehusishwa na tetesi za kutaka kujiunga na Newcastle baada ya kuondoka City, lakini bosi wa Chelsea Antonio Conte anamtaka kuziba pengo la Asmir Begovic, aliyejiunga na Bournemouth.

Post a Comment