WAKULIMA MKOANI SONGWE WAMEOMBA ELIMU KUTOLEWA KWANZA KABLA YA KULIMA
MBOZI:SONGWE
Wakulima wa
kikundi cha wakulima Ichenjezya Saccos wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameomba
kupatiwa mafunzo kwanza, kabla ya kuanza kulima na kupanda katika mashamba yao
ili ujuzi wanaopata wautumie kwa vitendo mashambani mwao.
Hayo yamesemwa jana katika kijiji cha Nselewa ambako
wakulima hao wamekutana kwa ajili ya mafunzo katika shamba darasa ambapo wamesema
licha ya kupatiwa mafunzo hayo lakini tayari sehemu kubwa wamekwishalima na
kupanda kwa mbinu walizozizowea jambo ambalo halijawasaidia sana.
Sekelo Kayange amesema kuanzia mwakani ni vizuri
wakulima wa kikundi hicho wakapatiwa mafunzo kwanza katika shamba darasa, kabla
ya kupatiwa pembejeo ndipo waendelee kuendeleza mashamba yao ili wataalamu
wanapotoa mafunzo ya namna ya kupanda kwa kutumia pembejeo za kisasa ili katika
muda ule ule waweze kutumia maarifa hayo kwenye mashamba yao ili kuleta tija.
Katibu wa kikundi cha Ichenjezya Joseph Masanja
amesema wazo la kupatiwa mafunzo mapema waliliona lakini walipowasiliana na
watu wa makampuni ya Mbegu walidai wasubiri mvua ziongezeke kwani kuanza
kupanda katika mashamba darasa wakati mvua ni chache zinaweza zisiote vizuri
kutokana na ukame lakini wakulima wakaona kama mbegu zao hazifai hazifai.
Wiki iliyopita Mkuu wa mkoa Songwe Chiku Galawa
akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake aliagiza wataalamu wa ugani
kuondoka ofisini na kuanzisha mashamba darasa katika maeneo yao ili wakulima wayatumie
kupata maarifa yatakayowasaidia kuboresha kilimo chao ili kuongeza tija na
kwamba hicho kitakuwa kipimo cha kila mgani.
Aidha Galawa alisema mkoa umeweka mkakati wa
kuongeza uzalishaji ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizaji wa pembejeo feki kwa
kuwatambua wasambazaji wa pembejeo kila eneo ambapo alisema mkoa unatarajia
kuongeza eneo la uzalishaji la hekta 299393 katika msimu wa kilimo 2017/2018
badala ya hekta 250117 zilizolimwa mwaka jana.
Post a Comment