KAMATI YA UCHAGUZI TFF YAKUTANA KUJADILI HATMA YA UCHAGU MKUU WA TFF
KIKAO cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kinachoketi leo Jumanne jijini Dar es Salaam, kimeshikilia shingo za wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho hilo sambamba na hatima ya mchakato wa uchaguzi mkuu ambao umesimamishwa, lakini huenda jambo kubwa zaidi likatokea leo.
Wakati
kikao hicho cha leo kikitajwa kuwa na lengo la kumaliza mpasuko
uliojitokeza kwenye Kamati ya Uchaguzi baina ya Mwenyekiti, Wakili
Revocatus Kuuli na wajumbe wake, habari ambazo gazeti hili limezipata ni
kuwa huenda kikao hicho kikaivunja kamati hiyo na kutangaza mpya.
Juzi
Jumapili, Wakili Kuuli aliamua kuusimamisha mchakato wa uchaguzi na
kuandika barua ya kuomba usaidizi wa Kamati ya Utendaji katika
kushughulikia mvutano ulioibuka kati yake na wajumbe wa kamati ya
uchaguzi juu ya zoezi la usaili na utangazaji majina ya wagombea
waliopitishwa na kamati hiyo.
“Mimi kama Mwenyekiti wa
kamati nimechukua jukumu na dhamana ya nafasi niliyo nayo kumuandikia
barua Katibu Mkuu wa TFF ikiwa dhamira yangu ni kuangalia upya mwenendo
mzima wa kamati. Nashukuru na yeye wamekaa na sekretarieti wamekubaliana
na maombi yangu na wameona ni sahihi mchakato huo usimame”, alisema
Kuuli juzi.
Hata hivyo taarifa ambazo gazeti imezinasa ni kuwa kamati hiyo ya uchaguzi ambayo iliundwa chini ya uongozi wa Malinzi, huenda ikavunjwa leo kutokana na mgawanyiko huo ulioibuka kwa wajumbe wake unaodaiwa kwa kiasi kikubwa kuchangiwa na mgongano wa kimaslahi.
KUMBE KUNA UKANDA?
Mgombea
wa nafasi ya Makamu Rais, Mtemi Ramadhani alisema: “Katika kamati ya
uchaguzi wajumbe watatu wanatoka mkoa ambao Rais anayemaliza muda wake
anatoka huko, lakini kama haitoshi kuna mjumbe mmoja anatoka katika
kamati tendaji ya mkoa wa Kagera kwahiyo hii inahatarisha kuwa na hali
ya kupendelea upande fulani, kwa hiyo maamuzi aliyoyafanya Mwenyekiti wa
kamati hiyo yapo sahihi kabisa.”
Mgombea mwingine wa
Makamu wa Rais, Robert Selasela alisema: “Kama Mwenyekiti anataka haki
itendeke halafu wajumbe wengine wanapinga hii haipo sawa na inaonesha
jinsi gani kuna mambo mengine ambayo siyo sahihi yanaendelea kati yao,
ila acha tuone kamati tendaji itaamua nini.”
KATIBA INASEMAJE?
Katiba
ya TFF kupitia Ibara ya 34 inatoa mamlaka kwa Kamati ya Utendaji ya
shirikisho hilo kuteua, kufanya mabadiliko ama kuchukua hatua dhidi ya
kamati mbalimbali zilizo chini yake ikiwemo Kamati ya Uchaguzi.
“Kamati
ya Utendaji ina Mamlaka ya kuteua wakuu wa idara za TFF na kuwachukulia
hatua za kinidhamu,” inasema ibara hiyo kwenye kifungu D wakati kifungu
J kinasema: “Kamati ya Utendaji ina mamlaka ya kuteua na kuwachukulia
hatua za kinidhamu, wajumbe wa kamati za kisheria, uchaguzi na za
kudumu.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa muda wa TFF, Salum
Madadi, hakuweza kukanusha wa kuthibitisha tetesi za kuvunjwa kwa Kamati
ya Uchaguzi na kudai kamati ya utendaji ndio itakayoamua.
“Kuhusu kipi kitafanyika kwenye kikao hicho, ni juu ya kamati, baada ya kukutana mtajua,” alisema.
Post a Comment