Header Ads


ZAIDI YA VIJANA 400 KUTOKA KATA ZA KEMAMBO MATONGO WILAYANI TARIME WAMEVAMIA MGODI WA NORTH MARA


TARIME-MARA
Zaidi ya vijana 400 kutoka kata za Kemambo Matongo Wilaya ya Tarime,
wamevamia mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia
wakishinikiza fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa na kampuni
hiyo kupisha uchimbaji wa dhahabu.

Hatua hiyo inahusishwa na ripoti ya pili ya kamati maalumu iliyoundwa na
Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini katika makontena 277.

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ilibaini kuwa kampuni ya Acacia
haitambuliki kwa kuwa haijasajiliwa rasmi nchini.

Akizungumza kwa simu jana, mkazi wa Kijiji cha Matongo, Adamu Kibe
alisema vijana hao walichukua hatua hiyo baada ya kuingiwa hofu ya
Acacia kuondoka au kufukuzwa bila wananchi kulipwa fidia kwa kuwa
haijasajiliwa.

“Kinachotutia hofu ni taarifa za kamati za uchunguzi za Rais Magufuli,
hasa ile iliyobaini kuwa kampuni hii haiko nchini kihalali kwa sababu
haijasajiliwa Brela,” alisema Kibe.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya lilizima
jaribio hilo kwa kuwatanya vijana hao kwa mabomu ya machozi na maji ya
kuwasha.

Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya, Andrew Satta alisema hakuna mtu
aliyeshikiliwa wala kujeruhiwa wakati wa tukio hilo lililotokea jana na
kudumu kwa zaidi ya saa moja.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Emmanuel Ngocho alisema vijana hao
walitoka katika vijiji vitatu vya Kewanja, Nyangoto na Matongo.

“Pamoja na ukweli kwamba vijana hawa ni wale wanaotafuta mchanga wa
dhahabu ili kujipatia kipato kutokana na hali yao ya kiuchumi kuyumba,
walijificha nyuma ya madai ya fidia ili kuhalalisha tukio hilo,” alisema
Ngocho.

Mkazi wa Nyangoto, Dominic Nyamohanga aliunga mkono kauli ya hali ngumu
kimaisha kuwa chanzo cha uvamizi wa vijana hao ambao lengo lao kuu
lilikuwa kupata mchanga wa dhahabu baada ya mgodi kusitisha kumwaga
mabaki ya mchanga kwa wananchi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Madai ya fidia

Tangu mwaka 2014, baadhi ya wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo
wamekuwa wakisubiri malipo ya fidia baada ya maeneo yao kuingizwa ndani
ya eneo la mwekezaji au kuhamishwa kupisha madhara yatokanayo na
shughuli za uchimbaji ikiwamo mitikisiko inayosababishwa na milipuko ya
baruti pamoja na vumbi.

Baadhi yao tayari wamelipwa huku wengine malipo yao yakichelewa kutokana
mvutano ulioibuka kuhusu tathmini na kiasi cha fedha ikilinganishwa na
thamani halisi ya ardhi na mali.

Akizungumzia vurugu hizo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Rashid
Bogomba aliwataka wakazi wa Nyamongo kuwa watulivu na kuepuka matumizi
ya nguvu kudai haki zao.

“Kila mtu, hasa sisi viongozi na wawakilishi wa wananchi tunapenda suala
hili la fidia lifikie mwisho kwa kila anayestahili kulipwa, lakini
matumizi ya nguvu ikiwamo kuvamia eneo la mwekezaji siyo njia ya sahihi
ya kudai malipo,” alisema Bogomba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya
Kemambo-Nyamongo.

Tangu mwaka 2010 baadhi ya wananchi walipofanyiwa tathmini ya ardhi na
mali zao, wahusika wamezuiwa kuendeleza au kufanya shughuli yoyote ya
kimaendeleo kusubiri fidia.

Mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo aliunda kamati iliyoshirikisha wawakilishi wa wananchi,
mwekezaji, viongozi wa maeneo yanayopakana na mgodi pamoja na wataalamu
kuchunguza kiini cha mvutano huo.

Akichangia hotuba ya bajeti kwa mwaka 2017/18 bungeni mjini Dodoma wiki
iliyopita, Mbunge Tarime Vijijini, John Heche alionya kuwa uvumilivu wa
wakazi wa Nyamongo kuhusu madhila wanayopata kutokana uwekezaji wa mgodi
wa dhahabu umefika mwisho.

No comments

Powered by Blogger.