MKUU WA WILAYA YA RUNGWE ATAKA WANAFUNZI WA KIKE WASIOKUWA TAYARI KUKAMATWA
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Julius Chalya |
RUNGWE-MBEYA
MKUU wa wilaya ya Rungwe Julius Chalya ameagiza kukamatwa na
kuwekwa ndani kwa wanafunzi wa kike ambao watagoma kuwataja wanaume waliohusika
kuwapa ujauzito.
Alitoa agizo hilo hivi karibuni wakati akifungua kikao cha
Wadau wa elimu katika halmashauri ya Wilaya hiyo cha kujadili na kuweka
mikakati ya kuinua kiwango cha elimu kwa shule za Msingi na Sekondari.
Chalya alisema baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakigoma
kutaja watu waliohusika kuwapa ujauzito kwa kuhofia wanaume wao watachukuliwa
hatua za kisheria.
Alisema pia wapo wazazi ambao wanashirikiana na wahusika
waliwapa ujauzito watoto wao na kumalizana wao kwa wao bila kufikisha suala
hilo mbele ya vyambo vya sheria hatua ambayo inapelekea ongezeko la Mimba za
anafunzi.
“Mzazi wa Kike na wa Kiume wakikubaliana kumaliza suala la
Mimba la mtoto wao bila kufikisha mbele ya vyombo vya sheria na mtoto wa kike atakayegoma
kutaja mhusika wawekwe wote,tukikaa kimya maana yake tumekubaliana na hali
hiyo,” alisema.
Hata hivyo aliwaagiza waratibu elimu katika kata zote za
halmshauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha wanasimamia mienendo ya walimu shuleni
kwa kuhakikisha wanawajibika ipasavyo na kuleta mageuzi ya kitaaluma katika
shule zao.
Pia aligusia suala la chakula shuleni ambapo alisisitiza kuwa
wazazi na Jamii kwa ujumla inapaswa kuwajibika kwa kuchangia chakula shuleni
kwa kuwa ni Muhimu katika kukuza ufaulu kwa wanafunzi.
Mkuu wa Chuo cha ualimu cha Mpuguso, Dorothy Mhaiki
alikumbusha kuwa lengo la kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa asilimia
kubwa linaitegemea sekta ya elimu.
Alisema sera ya viwanda inategemea kupata wataalamu mahiri wa
kusimamia na kufanya kazi kwenye viwanda hivyo watakaozilishwa kutokana na
Matunda ya elimu bora.
“Jambo la kufikia uchumi wa kati utakaotokana na nchi ya
Viwanda unategemea sekta ya elimu kwa kiwango kikubwa kuwa kuwa hiyo ndio yenye
jukumu la kutoa wataalamu watakaotumika kwenye viwanda, hivyo jambo la elimu
linahitaji uwajibikaji mkubwa,” alisema.
Afisa elimu Msingi katika Wilaya hiyo Joseph Mabeyo alikiri
kuwa suala la utoro kwenye shule za Msingi na Sekondari imekuwa changamoto
hivyo wadau wanapaswa kushirikiana kukabiliana na changamoto hiyo.
Post a Comment