Header Ads


WANANCHI WILAYANI KYELA MKOANI MBEYA WAMEUKATAA MRADI WA MAJI WA SHILINGI MILION 800





KYELA -MBEYA

WANANCHI wa vijiji vilivyopo kata ya Makwale wilayani Kyela mkoani Mbeya,wamejiapiza kulipokea Godauni la kuhifadhia mazao lililojengwa kwenye kitongoji cha Mwalesi kijiji na kata ya Makwale kwa gharama ya Milion 800 huku wakidai kuwa umejengwa chini ya kiwango,huku likiwa na nyufa zaidi ya 19 na sakafu ikibanduka.

Wakizungumza na gazeti hili,jana kijijini humo,kwa nyakati tofauti,walisema wakati mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2015 lengo ni kuhifadhi gunia 40,000 za mpunga,na wakati unaanza waliona madhaifu na kutilia shaka lakini wao kama wananchi waliambiwa wasihoji wanaotakiwa kuhoji ni viongozi wa halmashauri.

Erasto Mwangunguru mkazi wa Makwale,alisema hawapo tayari kulipoke jengo hilo kwa kuwa halitaweza kuhifadhi mazao yao kutokana na kuwa na nyufa nyingi huku sakafu yake ikipukutika na kwamba walipeleka malalamiko kwa viongozi wa kata ili wawajulishe viongozi ngazi ya wilaya.

Upendo Kwele,mkazi wa Mwalesi,alisema serikali ilikuwa na lengo zuri la kutaka kujenga godauni kwa lengo la kuhifadhia mazao kutokana na kata hiyo kuwa na mbuga kubwa ya kilimo cha mpunga lakini ujenzi wa jengo hilo upo chini ya kiwango licha ya kuwa wao si wataalam lakini pesa iliyotajwa ni kubwa.

Mwenyekiti kamati ya ujenzi wa skimu hiyo,Anyigulile Mwaipopo,alisema ni kweli na pia kamati yake inaungana na wananchi kulikataa jengo hilo na kibayo zaidi fedha ni kubwa,jengo linanyufa zaidi ya 10 licha ya wataalam kusema linapumua,lakini hawapo tayari kuona wanalipokea kwa kuwa halitakuwa na faida.

‘’Jengo linanyufa zaidi ya kumi,sakafu imebomoka,hatupo tayari kulipokea,tunahitaji wataalam wa ngazi za juu waje walikague na lifanyiwe marekebisho sehemu iliyokuwa na madhaifu,Milioni 800 ni pesa ndefu sana ukilinganisha na jengo lilivyo’’alisema Mwaipopo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Makwale Msafiri Mwambepo,alisema licha ya kuwa wao sio wataalam lakini jinsi jengo lilivyo halifanani na fedha iliyotajwa na kuwa wakati ujenzi unafanyika wao hawakushirikishwa hivyo alisema anaungana na wananchi kuukata mradi huo.

Diwani wa kata hiyo,Aliko Kasyupa alipohitajika kulizungumzia suala hilo hakuwa tayari  kwani alisema anaharaka kwenda kutumika katika majukunu mengine.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Dkt,Hunter Mwakifuna,alisema ni kweli suala hilo lipo,hata yeye alitembelea mradi huo na kubaini kuwa na nyufa 19 na sakafu ikiwa imebanduka na kwamba wakati mradi huo unajengwa yeye hakuwa mwenyekiti hivyo wametoa taarifa katika ngazi ya mkoa.

Alisema serikali imewapa fedha Mil,500 kujenga majengo katika kituo cha afya ambapo wamejenga majengo mapya 9 lakini Milioni 800 inayodaiwa kujenga jengo moja Godaun kunatia shaka,hivyo serikali kuu kupitia kamati ya bunge watakuja kufanya ukaguzi.

Kufuatia hali hiyo,kamati ya Bunge ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC),tarehe 19/01/2018 inatarajia kufika wilayani humo kufanya ukaguzi wa miradi ikiwemo godauni hilo lililozua utata.

Mradi huo umefadhiriwa na Benki ya Dunia mwaka 2014 na lilikamilika kujengwa mwaka 2015 na kampuni iliyopewa dhamana ya kujenga ni Shekemu Construction Co limited,Jv,wakishirikiana na kampuni ya Fair Classy Co,Limitedi kutoka mkoani Morogoro na ujenzi ulikuwa wa miezi 5.

No comments

Powered by Blogger.