Header Ads


JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA LIMETEKEZA MASHINE ZAIDI YA KUMI ZA MICHEZO YZ KUBAHATISHA









MBEYA
JESHI la Polisi mkoani Mbeya kwa kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), limekamata na kuteketeza zaidi ya mashine 10 za michezo ya kubahatisha zilizoingizwa nchini kwa njia za panya bila kulipiwa kodi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo lililofanyika katika Dampo la Jiji la Mbeya katika eneo la Nsalaga, meneja wa michezo hiyo nchini, Sadiki Elimsu, amesema mashine hizo zilikuwa zinatumika kwenye michezo bila kulipiwa kodi ya mapato.
Amesema mashine hizo zilikamatwa katika wilaya za  Chunya na Rungwe ambako zilikuwa zinatumika kwenye michezo hiyo kinyume na kanuni na sheria za nchi.
Aidha, Elimsu alisema waliamua kuziteketeza mashine hizo kutokana na kutokidhi viwango vya ubora vilivyowekwa katika kanuni na sheria za michezo ya kubahatisha nchini.
Ofisa Mkaguzi Mkuu wa GBT, Huseni Semvua amesema mashine hizo zilikuwa zinaiingizia serikali hasara ya Sh. milioni 5.16 kwa mwaka.
Ameongeza  mashine hizo zinasadikika kuingizwa nchini zikitokea China kupitia Zambia na kwamba hazikupita katika vituo vya forodha kwa ajili ya kukaguliwa na kuthibitishwa ubora wake.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Modestus Chambu, ambaye amesimamia zoezi hilo la uteketezaji wa mashine hizo amesema wataendelea kushirikiana na bodi hiyo kusaka mashine za aina hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaohusika.

No comments

Powered by Blogger.