MADUKA 200 YAPIGWA KUFULI KWA KUKOSA EFD MKOANI RUKWA
RUKWA
Meneja
wa TRA Mkoa wa Rukwa, Fredrick Kanyiriri, alisema jana kuwa, maduka hayo
yamefungwa baada ya kukaidi kutekeleza agizo la kuwa na mashine hizo ndani ya
wiki mbili.
“Tuliwapa
muda wa kutosha wanunue mashine hizo, lakini wengi wao hawajafanya hivyo kwa
hiyo TRA kwa kushirikiana na madalali waliopewa kazi hiyo, tumefunga biashara
zao hadi hapo watakaponunua EFD na kulipa faini kwa kutokutii sheria,” alisema.
Kanyiriri
alisema sheria inawataka wafanyabiashara ambao makusanyo yao kwa mwaka yanafika
Sh. milioni 14, kuwa na EFD ambazo zinapaswa kutumika kwa ajili ya kutolea
risiti pindi wanapofanya mauzo ya bidhaa zao.
Mashine
moja ya kielektroniki huuzwa kati ya Sh. 600,000 na 800,000 gharama ambayo, pia
inalalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara kwamba ni kubwa kulinganisha na
kipato chao.
Mmoja
wa wafanyabiashara ambaye ameathirika na sakata hilo, Tumbwene Kilale, alisema
kutokana na biashara kuwa ngumu kwa sasa, walipaswa kupewa muda zaidi kwa ajili
ya kujipanga, ili wanunue mashine hizo.
Aidha,
wakati mchakato huo ukiendelea. baadhi ya wafanyabiashara wamelazimika kufunga
wenyewe maduka yao na kukimbia kwenda kusikojulikana.
Hata
hivyo, Meneja Msaidizi Idara ya Ukaguzi wa TRA Mkoa, Amina Shamdas, alisema
kukimbia huko hakuwezi kuwa msaada kwao kwa kuwa sheria iko wazi watafungiwa
biashara zao na kutakiwa kuripoti ofisi za TRA na kulipa faini ya kati Sh. milioni
tatu na milioni 4.5.
Kwa
mujibu wa maofisa wa TRA, mkoa una wafanyabiashara 308 ambao wanapaswa kutumia
mashine hizo, lakini ni wafanyabiashara 108 tu wanaotumia kitu ambacho
kinafanya serikali kukosa mapato.
Post a Comment