Header Ads


JAFO AWATAKA WANANCHI MANZASE KUTUNZA MRADI WA MAJI.




 DODOMA 
 NAIBU  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Selemani Jafo amewataka wananchi wa kijiji cha Manzase, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kuhakikisha kuwa wanatunza miundombinu ya mradi wa maji ulioanzishwa kijiji hapo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.

 Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, katika ziara aliyoifanya ya  kukagua  mradi wa maji wa kijiji hicho, Jafo alisema iwapo wananchi hao watautunza mradi huo vizuri utawasaidia kwa kuwa wamepata taabu ya maji kwa kipindi kirefu.

 “Kumekuwa na kawaida ya baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo miradi ya namna hii imekuwa ikianzishwa kwa makusudi kabisa, wanaiharibu miundombinu ya miradi hii kwa kukata mabomba kwa makusudi  kwa lengo la kunywesha mifugo, kuiba vifaa mbali mbali kwenye mabomba na kuiba mitambo inayosaidia kusukuma maji” alisisitiza Jafo.

 Aidha, aliwataka Viongozi wote wa kijiji hicho kuhakikisha kuwa kamati ya maji ya kijiji ambacho ndicho chombo maalumu cha kusimamia maji katika ngazi ya kijiji kinasimamiwa ipasavyo.

 Alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi hao kujimilikisha miradi hiyo kwa kutumia fedha zinazokusanywa kwa matumizi yao wenyewe, na pindi miundombinu inapoharibika kijiji kinakosa fedha za kufanya marekebisho.

 Naye, Diwani wa kata ya Manzase  Steven Kwanga alisema, mradi huo wa maji utasaidia sana katika ukuaji wa uchumi wa wananchi wake kwani wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji.
Aidha alisema wananchi wamekuwa wakitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua maji badala ya fedha hiyo ingetumiwa kutimiza mahitaji mengine.


Jafo alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Mtera ,Livingstone Lusinde kwa kushirikiana na wananchi wake ambao wiki iliyopita aliambatana nao mpaka viwanja vya Bunge kuonana naye ambapo Naibu Waziri huyo aliwaelekeza wataalam wa Tamisemi na wataalam wa Halmashauri ya Chamwino kufanya Manunuzi ya haraka ya Jenerata ili mradi huo uweze kuanza kazi

 Mradi huo wa maji wa kijiji cha Manzase unatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote mwezi huu kwani mkandarasi wa mradi huo akishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI amekwisha ukamilisha kwa kiasi kikubwa na unatarajiwa kuhudumia idadi ya watu wasiopungua 8000

No comments

Powered by Blogger.