Header Ads


TAIFA STARS YAPANIA KUIFUNGA RWANDA KWAO




MWANZA
Taifa Stars inaondoka kesho Jumatano kuelekea nchini Rwanda tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan2018).
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Mwanza, Stars ilipata sare ya bao 1-1 na Rwanda hivyo italazimika kushinda au sare ya zaidi ya mabao mawili katika mchezo wa Jumamosi ijayoili kupata tiketi ya kusonga mbele.
Kocha Msaidizi wa Stars, Novatus Fulgence alisema wanaondoka nchini kwa lengo moja tu la kusaka ushindi na wanaamini watafanya vizuri.
Alisema makosa yaliyofanyika katika mechi ya kwanza benchi la ufundi liliyabaini na limeyafanyia kazi.

Alisema wachezaji wote wako fiti, isipokuwa beki Shomari Kapombe ambaye hadi leo Jumanne alikuwa bado hajakaa vizuri baada ya kuumia katika mechi iliyopita.
“Tunasafiri kesho Jumatano na nia yetu ni kupata matokeo mazuri kuhakikisha tunasonga mbele, vijana wana ari nzuri isipokuwa Kapombendio hali yake haijakaa sawa.. niwaombe watanzania kutuombea”alisema Novatus.

Nahodha Msaidizi wa Stars, Himid Mao alisema mazoezi waliyoyafanya wanaamini lolote linawezekana na kwamba kiu yao ni kupata matokeo mazuri na kusonga mbele.
“Sisi kama wachezaji kila mmoja hakufurahia matokeo ya mechi ile ya Jumamosi iliyopita, kwa sababu tulitarajia kushinda, lakini wenzetu wakaja kwa nia moja ya kupata sare, kwahiyo na sisi kule tunaenda kusaka ushindi”alisema Mao.
Kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya alisema kuwa katika mechi iliyopita Stars wangepata ushindi, lakini wapinzani wao walicheza kwa mbinu chafu ikiwamo kupoteza muda uwanjani na kuukosesha mpira ladha.

“Ninaimani tutapata ushindi,kwa sababu kama wao walikuja kwa lengo la kupata sare wakafanikiwa kwanini sisi tushindwe kule kwao?alihoji nyota huyo wa Simba.
 Kiongozi wa msafara wa huyo, Salum Umande Chama alisema Watanzania wawe na imani na timu yao kwani lazima waje na ushindi kutokana na morari waliyonayo vijana.
“Tunaondoka na msafara wa watu 29, ikiwa ni wachezaji 20 benchi la ufundi saba na viongozi wawili, lakini niwaombe watanzania kuwa na imani tunaenda kupambana ili kupata  ushindi,” alisema Chama.

No comments

Powered by Blogger.