QATAR YASIKITISHWA NA UAMUZI MPYA WA NCHI NNE ZINAZOISUSIA
Nchi nchi zikiongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Qatar zaongeza idadi ya wanaowaita magaidi wanaoshirikiana na adui yake Qatar
Qatar imesema kwamba uamuzi uliochukuliwa na nchi nne za kiarabu wa
kuyaorodhesha makundi 18 pamoja na watu binafsi wanaohusishwa katika
orodha yao ya magaidi ni hatua inayosikitisha na kushangaza.Badala yake
Qatar imesema kama nchi inafanya kila liwezekanalo kukabiliana na
itikadi kali.Kauli ya Qatar imekuja katika wakati ambapo leo Bahrain
imewashtaki watu 60 kwa tuhuma za kuunda kundi la kigaidi huku duru za
mahakama zikisema kwamba watu wote hao walioshtakiwa ni washia.Watu wote sitini wamepangiwa kusomewa mashtaka kwa pamoja tarehe 22 ya mwezi Agosti ambayo ni pamoja na kuunda kundi la kigaidi,kujipatia mafunzo ya kutumia silaha pamoja na miripuko kwa lengo la kufanya mashambulizi ya kigaidi na kudhamiria kwa makusudi kuua polisi nchini humo.
Kuhusu washtakiwa
Hayo ameyasema mwendesha mashataka wa serikali Ahmad al Hamadi.Lakini juu ya hilo ni kwamba washtakiwa 33 wameshaikimbia nchi hiyo ambapo inatajwa kwamba wengine wamekimbilia Iran,Iraq na Ujerumani na kwa maana hiyo watashtakiwa bila ya wao kuwepo mahakamani limearifu shirika la habari la serikali BNA. Ikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina duru ya mahakama imeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba watuhumiwa wote 60 ni washia.
Serikali ya Bahrain inaituhumu Tehran kwamba inachochea uhasama na upinzani katika taifa hilo dogo la kifalme ambalo lipo katika ghuba baina ya Saudi Arabia,Qatar na Iran.Ni hatua ambayo imechukuliwa na Bahrain katika wakati ambapo kuna mvutano unaoendelea kati ya nchi hiyo na washirika wake watatu dhidi ya Qatar wanayoituhumu kuunga mkono magaidi.Saudi Arabia,Misri,Umoja wa Falme za kiarabu na Bahrain zimeongeza makundi mengine 9 yenye makaazi yake Yemen na Libya pamoja na watu wengine tisa kutoka nchi kadhaa za kiarabu katika orodha ya magaidi zikisema wote ni washirika wa Qatar.
Sheikh Seif Bin Ahmed al Thani mkurugenzi wa ofisi inayohusika na masuala ya mawasiliano ya serikali ya Qatar amesema orodha hiyo mpya ni kitu cha kusikitisha na kushangaza ambacho kinafanywa na nchi hizo zilizoisusia Qatar kama mwendelezo wa hatua zao za kuipaka matope Qatar.Kwa mujibu wa afisa huyo wa ngazi ya juu wa Qatar hatua hii ambayo ndiyo ya karibuni kabisa ni ushahidi unaoonesha kwamba nchi hizo nne hazina malengo ya kujitolea kukabiliana na ugaidi.Suali hili la vikwazo linazungumziwa katika mtazamo takriban sawa ndani ya Qatar,
Mzizi wa Fitna
Nchi hizo nne zilikata uhusiano wake na Qatar Juni tano zikiituhumu nchi hiyo kwamba inayafadhili makundi ya kigaidi,kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine za kiarabu pamoja na kujiegemeza kwa Iran ambayo ni adui wao mkubwa.Nchi hizo nne zinaitaka Qatar kuukata uhusiano wake na Iran kuifunga kambi ya kijeshi inayotumiwa na wanajeshi wa Uturuki ndani ya Qatar sambamba na kukifunga kituo cha televisheni cha Al Jazeera ambacho kwa jicho lao wanasema kinazikosoa serikali zao.Juu ya hilo Qatar na Uturuki ni waungaji mkono wakubwa wa vuguvugu la Udugu wa kiislamu ambalo ni mwiba kwa watawala wa nchi hizo za kiarabu.Taarifa lakini ya nchi hizo nne,Bahrain,Misri Saudi Arabia na Umoja wa falme za kiarabu iliyotolewa jana Jumanne inawatuhumu raia wa Qatar Kuwait na Yemen kwamba wanasaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasainia wapiganaji wa Al Qaeda.
Imeandaliwa na Mwandishi:Saumu Mwasimba
Post a Comment