MGHIRA AANZA KUWAVAA WAPINZANI
KILIMANJARO
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna
Mghwira amesema kuwa njia aliyoitumia aliyekuwa mgombea kiti cha urais katika
uchaguzi mkuu uliopita kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), na Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ilikuwa ni aina fulani ya ufisadi wa
kisiasa.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki
wakati akifanya mahojiano na Gazeti la Mwananchi ambapo amesema kuwa Mjumbe
huyo wa Kamati Kuu ya Chadema njia aliyoitumia ilikuwa ni aina mojawapo ya
ufisadi kwakuwa hakupitishwa na chombo chochote ndani ya chama chake.
Amesema kuwa hata katika Kampeni za
uchaguzi mkuu, Ukawa haikuzungumzia suala la ufisadi kwakuwa kiongozi huyo
teyari alikuwa ameshajiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Kwenye Kampeni za mwaka 2015 chama
kikuu cha upinzani (Chadema) hakikuwa tena kinazungumzia suala la ufisadi,
labda kwa hofu kuwa mshtumiwa wa ufisadi alikuwa mgombea wao, kwa bahati mbaya
wao ndio waliibua tuhuma za ufisadi, lakini kuondoka kwa Dkt. Slaa nako
kulikuwa ni tatizo, ingawa watu hawakutaka kulifuatilia,” amesema Mghwira.
Aidha, Mghwira amesema kuwa watu
walitakiwa kuhoji sababu za kuondoka kwa Dkt. Slaa na alikoelekea, nakuongeza
kuwa ni ajabu kwa kiongozi anayepigania demokrasia anaingia kwenye chama na
kugombea nafasi ya urais bila kupitishwa chombo chochote.
Hata hivyo, Mghwira ambaye ni
kiongozi wa kwanza wa upinzani kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa tangu kurejea
kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, amesema kuwa njia waliyotumia Chadema si
tu inarudisha nyuma siasa za upinzani, bali haikutoa picha nzuri ya demokrasia
ndani ya upinzani.
Alikerwa kuvuliwa uenyekiti
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika
nyumbani kwake Shanty Town mjini Moshi, Mghwira alikumbuka karaha aliyoipata
baada ya furaha ya kuaminiwa na Rais na kupewa wadhifa huo.
Alisema kama si ubabaishaji wa
kisiasa Tanzania, asingeondolewa kwenye uenyekiti wa ACT-Wazalendo.
“Changamoto niliyokutana nayo
ACT-Wazalendo kama mwenyekiti ni kukosa wigo sahihi wa kisiasa kwa sababu kama
tungekuwa tunafanya siasa sahihi, nisingeondolewa uenyekiti,” alisema.
Mghwira alisema, “Naapishwa tu kuwa
RC (mkuu wa mkoa) kesho yake naondolewa tena tukiwa tumepanga kukutana kwenye
kikao na mpaka leo hatujawahi kukutana.
“Nimesoma kwenye magazeti kuwa
mrithi wa Mghwira kutembelea mikoa saba, yaani na mrithi ameshapatikana. Hizo
si siasa, huo ni ubabaishaji. Ubabaishaji wa kisiasa Tanzania ni tatizo,”
alisema.
Aliongeza, “Sisi kina mama
tukisimama imara tunaweza kuondoa dhana hii ya siasa za ubabaishaji. Ni siasa
za kipuuzi kabisa. Mmekubaliana mkutane muongee, hamuongei wenzako wanakaa
pembeni. Umechaguliwa na mkutano mkuu unaondolewa na kamati ndogo. Watu 370
karibu 400 hivi walikuchagua, siku ya kuondolewa unaondolewa na watu watatu au
wawili au mmoja. Hiyo si siasa ni dalili tosha kuwa hakuna siasa.”
Alisema mbaya zaidi ni kuwa watu
wanaokuondoa hawakutumwa na mkutano mkuu, wala hawakukaimishwa na kamati kuu.
Hakuna upinzani nchini
Baada ya kujumuisha yote hayo na
hasa alivyotimuliwa kwenye uongozi, mkuu huyo wa mkoa akawa na jibu moja kuhusu
siasa za upinzani, “Hakuna siasa za upinzani, bali zilizopo ni za kurudishana
nyuma maendeleo.
“Siasa ni kitu kizuri kwa maana ya
ile mijadala, kubadilishana mawazo na kuzungumzia masuala ya itikadi, mipango
ya kijamii... hakuna hiki kitu Tanzania.”
Badala yake alisema, “Tumeweka siasa
kama ni uhasama kati ya chama tawala kilichoshinda kihalali na vyama hivi
vingine. Kila siku watu wanatafuta makosa ya wenzao (Serikali) hata kama
inafanya vizuri. Hiyo sio siasa.
“Vyama vya upinzani hapa hatuendeshi
siasa. Awali, chama chochote kitakachoibuka na siasa inayoeleweka kinaweza
kutawala nchi hii kwa miaka 100 ilimradi tu kitoke na siasa inayoeleweka.”
Mghwira alisema, “Vikitokea vyama
vitatu vinaendesha siasa inayoeleweka tunakuwa mahali pazuri zaidi. Kwa maana
kwamba wale wakiongea jambo lao, hata kama hawatawali, mtawala asikie na
kuthamini.
“Sisi hapa Tanzania kuna aina ya
siasa za kudidimizana. Kwa sisi wanawake wanaharakati tunaziita PhD (pool her
down). Unavutwa tu chini hutakiwi kukua. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.”
Alisisitiza, “Kuna watu wanafikiri
kwamba ili kitu kiwe sahihi ni lazima wao wakifanye (upinzani) lakini
kikifanywa na watu wengine hakiko sahihi. Hiyo ni kutokuwa mwanasiasa. Kuwa
mwanasiasa si kugombana ni kuwa na uwezo wa kujenga hoja, kuitetea na
kuisimamia. Mwenzako akija na hoja kubwa zaidi kubali.”
Post a Comment