Header Ads


NEC YATUMIA HOJA 6 KUIKANDAMIZA CHADEMA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesisitiza kuwa itaendelea kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili na taratibu mbalimbali katika kuendesha chaguzi nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani  wakati akijibu shutuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mhe. Freeman Mbowe juzi, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii NEC haikutoa ushirikiano kwa Chama hicho na kwamba ilikiuka Sheria na taratibu za Uchaguzi katika kuendesha Uchaguzi Mdogo uliofanyika Februari 17, 2018.

“ Ni kwamba shutuma na malalamiko yaliyotolewa na Mhe, Mbowe yametusikitisha kwa sababu mbali na kumjibu kwa barua, tuliongea naye kwa njia ya simu. Haya  madai kwamba Tume haikuyajibu malalamiko yao sio kweli, ni upotoshaji wa hali ya juu ambao haupaswi kufanywa na kiongozi kama yeye” Alisisitiza Kailima.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijibu malalamiko kwa kuzingatia  matakwa ya mtu bali inajibu hoja kwa mujibu matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na Maadili ya uchaguzi pamoja na maelekezo yote ambayo yapo kwa mujibu wa sheria.

Alieleza kuwa Kanuni, sheria, maelekezo na maadili ya Uchaguzi yameweka utararatibu wa kushughulikia malalamiko na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa uchaguzi ,uteuzi, na wakati wa kipindi cha kampeni ambapo malalamiko yote hushughulikiwa  na Kamati za Maadili zilizo katika maeneo husika ya uchaguzi kuanzia ngazi ya Kata, Jimbo na Rufaa.

“Kwa masikitiko CHADEMA walitekeleza hatua moja tu katika vipengele hivyo wakati wa uchaguzi, kipengele walichotekeleza ni pale baadhi ya wagombea wao walipoenguliwa kugombea, walifuata utaratibu kwa kuwasilisha rufaa Tume ya uchaguzi na Tume ilipitia na ikawarudisha wagombea wao kwenda kugombea” Alisisitiza Kailima.

Alibainisha kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilitaka wakati wa kampeni Tume ifanye maamuzi kinyume cha maadili waliyoyasaini akisisitiza kuwa kamati za maadili ngazi ya jimbo ambazo Mwenyekiti wake ni Msimamizi wa Uchaguzi na wajumbe wake ni kutoka vyama vyote vilivyosimamaisha wagombea ndio wanaofanya uamuzi.

Aidha, alisema CHADEMA  waliwasilisha malalamiko kwa Tume badala ya kuwasilisha malalamiko kwenye kamati hizo za maadili zinazosimamia malalamiko yote. 
“ Sio sahihi kusema Tume hatukujibu malalamiko yao. Mfano tarehe 15 Chadema waliwasilsiha barua mbili Tume ya Uchaguzi, waliwasilisha barua moja asubuhi na saa 1.30 jioni waliwasilisha barua nyingine, jumla barua hizo zikiwa na hoja tano na Tume ikawaandikia barua zenye ufafanuzi wa hoja hizo”

Akitoa ufafanuzi kuhusu hoja zilizowasilishwa na CHADEMA alisema kuwa Chama hicho kilitaka Mawakala wao mbadala ambao ni asilimia 15 waapishwe hatua iliyoifanya NEC iwajibu kwamba hakuna kifungu cha Sheria kinachotoa fursa kwa chama chochote cha siasa kuapishiwa mawakala mbadala asilimia 15.

“ Ukisoma Kifungu cha 57 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi  kinafafanua vizuri namna ya mawakala wanavyotakiwa kuwepo na kuapishwa lakini pia hata kama kifungu hicho kingekuwa kinatoa fursa hiyo, Chadema walileta malalamiko yao  tarehe 15 Februari 2018 wakati muda wa uteuzi wa mawakala ulikuwa tarehe 10 Februari 2018, hivyo hakukuwa na muda wa kuwaapisha mawakala wengine kwa mujibu wa sheria kwa kuwa hawakuwemo kwenye orodha” Alisisitiza.

Hoja nyingine iliyowasilishwa na CHADEMA ni ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni alikataa kuwapa mawakala barua na fomu za viapo.  
“Kuhusu hoja hii tulifanya hesabu tukaona kwamba msimamizi alitakiwa kusaini barua 22,000 na fomu za viapo 14,000. Tukasema kwamba kutakuwa na utaratibu wa mawakala kupewa fomu na viapo vyao kupitia kwa wawakilishi wao na walipewa kwa njia hiyo,  Hili tuliwajibu hivyo katika barua yetu” Alibainisha Kailima.

Kuhusu Mawakala wa CHADEMA kuambiwa kwenda na vitambulisho kwenye vituo vya kupigia kura NEC iliwajibu kwamba wakala chama cha siasa ni mpiga kura kama walivyo wapiga kura wengine.
 Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia sheria ya uchaguzi kifungu namba 61 na namba  62 cha sheria za Serikali za Mitaa ilitoa ridhaa kwa wapiga kura kutumia vitambulisho mbadala ili nao waweze kupiga kura ndio maana wakaelekezwa kwenda navyo.

Hoja nyingine ni kwamba msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, hajatoa maelekezo ni wapi pa kuhesabia kura ambapo walijibiwa kwamba Tume ina barua kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi akiwajulisha vyama vya siasa kwamba sehemu ya kujumlishia kura itakuwa ni sehemu ya Biafra.

“Kanuni inasema wangejulishwa eneo hilo la kujumlishia baada ya kura kupokelewa, lakini msimamizi wa uchaguzi aliwajulisha mapema eneo la kujumlishia kura” Alisema.

Hoja nyingine iliyotolewa inahusu Wasimamizi wa vituo hawakuteuliwa kwa utaratibu. Majibu ya hoja hii ni kwamba sheria ya uchaguzi imeweka utaratiibu wa namna wasimamizi hao wanavyopatikana. Lakini kanuni za uchaguzi wa Rais namba 15 na kanuni 11 za Serikali za Mitaa zinaeleza namna msimamizi wa kituo anavyopatikana.

Kanuni hiyo inasisitiza kuwa msimamizi wa uchaguzi atatoa tangazo, Kwa jimbo la Kinondoni msimizi alitoa tangazo, watu waliomba, walifanya usahili na kabla ya uteuzi mkurugenzi wa uchaguzi alitoa matangazo ya majina katika mbao zote za kata 10 za jimbo la Kinondoni.

Aidha, alisema kuwa Msimamizi wa uchaguzi aliwaandikia barua vyama vyote kama vina pingamizi vijitokeze. Kama kulikuwa na tatizo vyama vilikuwa na fursa ya kuweka pingamizi, lakini hawakufanya hivyo na Tume iliwajibu hivyo. Wanaposema Tume haikuwajibu sio kweli  labda  waseme walijibiwa nje ya matakwa yao  na sio kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu hoja ya wizi wa kura ameeleza kuwa katika kituo cha kupigia kura kuna Msimamizi wa kituo, Msimamizi msaidizi na Wakala wa chama cha siasa na kuna waandishi wa habari hivyo hakukua na fursa ya jambo hilo kutokea.

Alisema utaratibu wa upigaji wa Kura ulikuwa wazi na kusisitiza kuwa kuna utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha malalamiko kama mtu haridhiki kabla wakati na baada ya kupiga kura, wakati wa kuhesabu na baada ya kuhesabu kura.

Mkurugenzi Kailima alieleza kuwa mtu au chama kisipofuata uratibu huo, lazima kitailalamikia Tume na Mgombea akikataa kufuata utaratibu huo hata akija Tume kulalamika,ataelekezwa na Tume atumie wakala wake kujaza fomu zote namba 14 na 16 zinazohusika kisheria kuwasilisha malalamiko.

“Tunamsihi Mbowe na chama chake, wasome sheria za uchaguzi na kuzielewa. Tume iko tayari kumpa elimu ya mpiga kura kuzifahamu sheria hizi kwa mapana yake, Pia tunamwomba Mhe. Mbowe kama hakuridhika na taratibu za uchaguzi, ana fursa ndani ya siku 30 za kuwasilisha malalamiko yake Mahakamani ambacho ndicho chombo pekee cha kutoa haki’” Alisisitiza 

Amekitaka Chama hicho kwenda Mahakamani kwa kutumia ushahidi ambao Mawakala wake walijaza kwenye fomu namba 14 na 16 kwa sababu Tume ya Uchaguzi haina tena fursa ya kupokea malalamiko kisheria baada ya uchaguzi kupita.
 

No comments

Powered by Blogger.