Header Ads


WAKAZI WA KIJIJI CHA MAWINDI WAISHUKURU SERIKALI KWA KUWAPELEKEA ZAO LA KOROSHO

MBARALI-MBEYA
WAKAZI wa Vijiji vilivyopo katika kata ya Mawindi wilayani Mbarali,wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea zao la Korosho wakisema kwa miaka mingi hawakuwa na zao la biashara.

Wakazi hao wamesema kutokana na eneo lao kutofaa kwa kilimo cha zao la Mpunga kwa miaka yote wamekuwa wakilazimika kulima mahindi na mazao mengine kama alizeti na karanga ambayo hayajawa na faida kubwa kwao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mkandani kata Mawindi,Sadick Kimelei,alisema kufika kwa zao la Korosho kijijini kwao ni Mafanikio mengine makubwa kiwilaya kwakuwa wakati wakazi wakiendelea na shughuli nyingine watakuwa sasa wakisubiri baada ya miaka kadhaa kuanza kunufaika na Korosho.

“Haya ni mafanikio makubwa kiwilaya,kwa kijijini kwangu hatulimi mpunga kama maeneo mengine wilayani hapa.Nitakuwa kioo cha jamii ili wananchi wangu wapate matumaini kutoka kwangu.Nata kuona nakuja kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kunufaika na zao  hili.”alisema Mwenyekiti huyo wa kijiji.

Hata hivyo Kimelei aliuomba uongozi wa wilaya na wataalamu wa kilimo kuwatembelea mara kwa mara kijijini kwao ili kuwapa hamasa zaidi wananchi juu ya kilimo cha zao hilo.


Kwa upande wake Afisa ugani wa kijiji cha Manienga kilichopo katika kata hiyo,James Mgaya alisema baada ya wanakijiji kupata taarifa ya uwepo wa miche ya korosho inayogawiwa bure,wamehamasika kwa wingi na kila moja anataka kupanda zao hilo.

Nae Afisa ugani wa kata ya Mawindi,Samson Risbon alisema wananchi wa vijiji vyote vitano vya kata hiyo wamepokea zao hilo na tayari wakulima 86 wameandaliwa kuanza kupanda miti kwenye maeneo yao.

No comments

Powered by Blogger.