MKUU WA MKOA WA MBEYA AWAAGIZA WAKUU WA WILAYA KUHAKIKISHA MITI INAPANDWA KATIKA WILAYA ZAO
Mkuu wa mkoa wa mbeya Amos Makala |
MBEYA
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema Mpango wa Kitaifa wa kuhakikisha miti milioni
moja na nusu kila Halmashauri inapandwa hauwezi kufanikiwa iwapo viongozi wa
kiserikali hawatowashirikisha kwa karibu wananchi.
Kufuati hali hiyo,mkuu huyo wa mkoa amewaaagiza
Wakuu wa Wilaya kutumia msimu wa mvua kuhamasisha wananchi kupanda miti ili
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makalla alitoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa Kampeni
ya upandaji miti Kimkoa iliyofanyika katika Mtaa wa Ilembo Kata ya Mwansekwa
jijini Mbeya.
Alisema Wakuu wa Wilaya wanatakiwa kuhakikisha wanawahimiza wananchi kupanda
miti na kuwapa uelewa wa umuhimu wa utekelezaji wa malengo ya Kitaifa ya
kupanda miti.
Alisema iwapo viongozi na wataalamu watajifungia
maofisini na kujipangia wenyewe matukio ya upandaji miti,wananchi watabaki
kuamini kazi hiyo haiwahusu na kuona ni jukumu la Serikali pekee jambo
litakalochelewesha kufikia malengo.
“Lengo la kampeni ya kitaifa ni kuwashirikisha
wananchi ili wawe na tabia ya kupanda miti ili kukabiliana na uharibifu wa
mazingira pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.Wajue umuhimu wake. Na
wabadilike kwa kila mmoja kuona fahari pale anapopanda miti na kuitunza”
“Tunataka kuchochea uendelezaji na uhifadhi wa
mazingira yanayomzunguka binadamu katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.Kila
mtu anapaswa kutoharibu ama kuchafua vyanzo vya maji.”alisisitiza Makalla.
Aidha aliwataka wananchi kuepuka kusababisha moto na
kudhibiti uchomaji moto misitu, ufugaji ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na
kutoa taarifa kwa mamlaka juu ya tukio linaloweza kuhatarisha uhifadhi wa
maliasili na viumbe hai.
Awali Mwenyekiti wa Sekretarieti ya utekelezaji wa
mpango wa hifadhi wa safu za Mlima Mbeya, Venance Hawela alisema katika
utekelezaji wa kampeni hiyo, Mradi umejiwekea malengo ya kupanda miti 102,000
kwa mwaka 2017/2018.
Hawela alisema miti iliyolengwa kupanda ni pamoja na
miti 82,000 kwa ajili ya vyanzo vya maji, 20,000 kwa ajili ya mapambo, matunda
na vivuli ambayo itapandwa kandokando ya barabara kuu ili kupendezesha Jiji la
Mbeya.
Kwa upande wao Machifu wa kabila la Wasafwa Chifu
Mwanjajila Mwambanje na Katibu wa Machifu Mwanamtwa Yilanga walitoa wito kwa
wananchi kuhakikisha kila mwenye shamba anapanda miti na kuitunza na kwamba ambaye
hatatekeleza agizo hilo atachukuliwa hatua kali.
Post a Comment