Header Ads


TAHARUKI YATANDA UKOSEFU WA CHOO STENDI KUU KYELA





KYELA-MBEYA
ZAIDI ya watu 2,000 wanaoingia na kutoka katika stendi kuu ya Kyela mkoani Mbeya, wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko baada ya kukosa huduma ya vyoo huku wakijisaidia pembezoni mwa stendi hiyo, baada ya choo kilichopo kujaa na kukosa sehemu ya kujisitili.

Akizungumza jana hali hiyo Babu Masangula ajenti wa mabasi ya Kyela Express, alisema ni muda mrefu sasa tangu choo hicho kujaa huku abiria ambao wanalala katika stendi hiyo wakikosa sehemu ya kujisitili huku wengine wakijisaidia pembezoni mwa stendi hiyo na kuchafua mazingira.

Jofrey Kyando ajenti wa New Force, alisema choo kimejaa na walipeleka malalamiko kwa viongozi husika lakini hakuna kinachoendelea na kwamba kutokana na watu kujisaidia pembezoni mwa stendi hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka magonjwa ya mlipuko kwa kuwa mama lishe wanauza vyakula katika eneo hilo.

Anna Msumari mama lishe katika stendi hiyo alisema choo kimefungwa kutokana na kujaa hivyo wanalazimika kwenda soko kuu kujisaidia nyakati za mchana, usiku wengi hujisaidia kwenye mfereji unaozunguka stendi hiyo, licha yakuwepo ya faini ya 50,000/- kwa anayebainika.

Vellina Mwandali mmiliki wa choo hicho alikiri choo chake kujaa na kusema kuwa siku saba zilizopita alitoa taarifa kwa mtendaji mkuu wa mamlaka wa mji mdogo (TEO) ambaye alimueleza atamuonyesha sehemu nyingine ya kuchimba ili huduma iendelee.

Akizungumzia hali hiyo Diwani wa kata ya Mbugani, Claud Fungo alikiri kuwepo kwa adhaa hiyo na kusema kuwa atawasiliana na mamlaka husika inayohusiana na mambo ya afya ili kutafuta uvumbuzi wa suala hilo ili kuokoa maisha ya watu.

Mtendaji mkuu wa mamlaka wa mji mdogo (TEO) Rafael Samwel alipofuatwa ili kuzungumzia suala hilo hakuweza kutoa ushirikiano akidai kuwa ametoka kwenye kikao amechoka na kuahidi kuwa atalizungumzia siku nyingine.

Mwenyekiti wa mamlaka wa mji mdogo wa Kyela, Josephat Longoli alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa kesho atazungumza na Afisa Mtendaji mkuu wa wa mamlaka wa mji mdogo kwa kushirikiana na idara ya afya ili kuweza kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

No comments

Powered by Blogger.