ASLIMIA 28 YA WANANFUNZI WANAOMALIZA DARASA LA SABA HAWAWEZI KUFANYA MAJARIBIO YA KUSOMA NA KUFANYA HESABU ZA DARASA LA PILI
TUNDUMA -MOMBA- SONGWE
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Uwezo
iliyopo chini ya Twaweza unaonesha asilimia 28 ya wanafunzi wanaomaliza darasa
la saba hawawezi kufanya majaribio ya kusoma na kufanya hesabu za kiwango cha
darasa la pili, huku asilimia 48 wanamaliza elimu ya msingi wakiwa hawajui
lugha ya kingereza.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na mratibu wa
Uwezo mkoa wa Mbeya Furaha Christopher alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi
wa ripoti ya halmashauri ya Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe, kuhusu utafiti
uliofanywa na taasisi yake kwa kusaidiana na shirika la (ADP)Mbozi kuwa takribani watoto 6 kati ya 10 wa darasa la
tatu sawa na asilimia (56) waliweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la
pili.
Alisema Kwa darasa la saba, watoto 9 kati ya 10 sawa
na asilimia 89, waliweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili, hali
ambayo inamaanisha takribani asilimia 11 ya watoto wanamaliza darasa la saba
bila kujua kusoma na kuandika.
Christopher alisema mtoto 1 tu kati ya 10 sawa na 13 wa darasa la
tatu alioweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili, kwa darasa la
saba, ni takribani watoto 5 kati ya 10 sawa na asilimia 48 waliweza kusoma
hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili idadi ambayo ni karibu nusu ya
wanafunzi wa darasa saba wanamaliza shule bila kuwa na maarifa muhimu ya lugha
ya Kiingereza ambayo ni lugha ya kufundishia sekondari.
Aidha alisema utafiti
huo ulifanyika mwaka 2015 na kuhusisha wilaya zote 159 Tanzania bara, (vitongoji)
30 kwa kila wilaya, (jumla 4,770), Kaya 20 kwenye kila kijiji au Mtaa, hivyo ni
kaya 600 kila wilaya na mbinu iliyotumika ni kuwahoji wanafunzi wenye kati ya
umri wa miaka 7 na 16 kwa kuwapa majaribio ya darasa la pili ya hesabu, kusoma
Kiswahili na kingereza.
Mgeni rasmi katika
hafla hiyo ambaye pia ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Majengo Kulthum
Njalambaha alisema zipo sababu nyingi zinazoathiri watoto kujifunza shuleni
ikiwa ni pamoja na mrundikano wa watoto darasani ambao unaathiri mwalimu
kuwafikia wote ili kuhakikisha kama wameelewa wanachofundishwa.
Alisema sababu nyingine
ni ushirikiano hafifu kati ya walimu na wazazi ambapo baadhi ya watoto ni
watoro wasiohudhuria vipindi vyote darasani kwa visingizio mbalimbali kama
kukosa mahitaji muhimu kama daftari na kalamu, na kukosa chakula cha mchana.
Njalambaha aliitaka
jamii kuendelea kujenga vyumba vya madarasa ili kupunguza mlundikano wa
wanafunzi darasani ili uwepo uwiano unaostahili wa watoto 45 kwa mwalimu mmoja
badala ya uwiano uliopo sasa kwa shule nyingi wa zaidi ya watoto 100 ambao
walimu wanashindwa kuwafikia wote.
Mmoja wa wanafunzi wa
darasa la tano katika shule ya msingi Majengo Gollani Ansa alisema serikali iwasaidie kuwapatia walimu
wa masomo ya hesabu na kingereza kwani waliopo ni wachache na mkazo ni mdogo.
Bensoni Mlowezi ni
mzazi ambaye alisema ili kuongeza ufaulu
wa watoto wao lazima mahusiano ya karibu kati ya wadau hao watatu, mwalimu
mzazi na mwanafunzi ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, kuanza kutoa
chakula cha mchana kwa wanafunzi.
Afisa mtendaji wa mtaa
wa Half Londoni Maua Isaya alisema wakazi wa Tunduma wamejiingiza zaidi kwenye
masuala ya biashara huku wakisahau masuala ya elimu kwa watoto wao, ambapo
wakati Fulani wakiitwa na ofisi yake au mwalimu shuleni wamekuwa wakituma
vijana wa kazi za nyumbani watu ambao ni vigumu kutoa mamuzi.
Mkuu wa mkoa wa Songwe
Chiku Galawa tayari ameagiza shule zote mkoani hapa kuanza kutoa chakula cha
mchana kwa wanafunzi ikiwa ni njia ya kupunguza utoro unaotokana na njaa na
kuongeza ufaulu kwa kuziagiza halmashauri zote zihakikishe wazazi wanachangia
chakula kwa watoto wao.
Aidha jitihada hizo pia
za ujenzi wa vyumba vya madarasa zinaendelea kufanyika ili kupunguza mlundikano
wa watoto madarasani, mkoa wa Songwe katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka
huu imekuwa miongoni mwa mikoa 10 iliyofanya vibaya .
Mwisho
Post a Comment