ASILIMIA 80 WANANCHI WA MKOMBA WANAUGUA HOMA ZA MATUMBO KWA KUNYWA MAJI YASIYOSALAMA
MOMBA-SONGWE
ASILIMIA 80% ya wananchi wa vijiji
vya Chole na Mkomba kata ya Mkomba wilaya ya Momba mkoani Songwe wanaugua homa
za matumbo ikiwemo kipindupindu na kuhara kutokana na tatizo la kukosekana kwa
maji safi na salama kwa muda mrefu.
Wakizungunza jana na gazeti hili
walisema wanalazimika kutumia maji machafu yasiyo salama ambayo hata hivyo
hayapatikaniki kirahisi hivyo kuiomba serikali katika bajeti yake ya mwaka
2017/2018 itoe kipaumbele vijijini katika kutatua kero ya maji.
Menance Maarifa mkazi wa kijiji cha
Chole,alisem kwa kuwa serikali imetenga billion 1.6 kutatua kero ya maji katika
halmashauri ya wilaya ya momba, ambapo wameomba serikali itoe kipaumbele zaidi
vijijini,kikiwemo kijiji cha Chole,na kutimiza lengo la kumtoa mama ndoo
kichwani.
Ester Sichimbo,mkazi wa
Mkomba,alisema ndoa zao zipo rehani kutokana na kugombana na waume zao pindi
wanapochelewa kurudi nyumbani kwakuwa wanatoka alfajiri kwenda kutafuta maji na
kurejea nyakati za jioni hivyo wamekuwa wakipigwa na kusababisha ndoa zao
kuyumba.
Mwenyekiti wa kijiji cha Chole
Damian Sichila,asilimia 80 ya wananchi wake wanaugua homa za matumbo na kwamba
hata serikali ikija kuwapima watabaini hayo,na kuwa endapo bajeti ya mwaka huu
serikali itakiangazia kijiji chake kuondoa kero ya maji tatizo hilo litakwisha
na hatakesi za ndoa hazitakuwepo.
Diwani wa kata ya Mkomba Colletha
Mwanselela alisema katika vitongoji 25 kwenye kijiji cha Chole ni kitongoji
kimoja tu chenye unafuu wa maji huku vingine 24 havina maji na kuongeza kuwa
katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kata ya Mkomba ilitengewa fedha za maji
million 16 lakini hazikutolewa, hivyo kuiomba halmashauri kuhakikisha bejeti ya
mwaka huu inatekelezeka.
Juma Irando,mkuu wa wilaya
hiyo,alisema kutokana na kuwepo kwa kero hiyo kwa muda mrefu amemuagiza
mkurugenzi mtwndaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha anapeleka fedha kwenye
kijiji hicho kwa kuwa tayari Momba imetengewa Bilioni 1.6.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri ya wilaya ya Momba,Maua Mgalla,licha ya kukiri kuwepo na tatizo
hilo,aliosema katika bajeti ya mwaka huu kijiji hicho kitapewa kipaumbele ili
kiondokane na kero hiyo.
Mathew Chikoti,Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo,alisema ni kweli kijiji hicho kinakabiriwa na ukosefu wa maji
na kwamba katika bajeti ya mwaka huu atahakikisha Chole inapewa fedha za miradi
ya maji na kuwa kutokana na wananchi wa kijiji hicho kuumwa magonjwa ya homa za
matumbo,atawaagiza madaktari kwenda kuwapima na kuwapa tiba kesho kutwa.
Post a Comment