MKUU WA MKOA WA MBEYA bW. AMOS MAKALA APOKEA MSAADA WA MADARASA
MKUU wa Mkoa wa Mbeya,Amos Makalla amepokea vyumba
viwili vya madarasa na kimoja cha Ofisi ya walimu vilivyojengwa kwa msaada
mkubwa wa Kampuni inayojishughulisha na unuzuzi wa zao la Kakao wilayani Kyela ya
Kim’s chocolate(Belgium) Bioland International katika Shule ya msingi Ngana
iliyopo wilayani hapa.
Makalla pia amepokea madarasa vyumba viwili vya
madarasa vilivyojengwa na Kampuni hiyo katika Shule ya Msingi Lubele iliyopo
katika kata ya Ikimba.
Kwa mujibu wa Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kyela,Mwalimu Polemone Ndarugiliye ujenzi wa vyumba vitatu katika
shule ya msingi Ngana ulioambatana na ukarabati wa vyumba vingine viwili shuleni
hapo uligharimu Shilingi 23,271,000 ambapo kampuni ya Bioland ilichangia
Shilingi 17,000,000 sawa na asilimia 73.1,wananchi Shilingi 5,128,000 sawa na
asilimia 22 kupitia nguvu kazi.
Mwalimu Ndarugiliye alisema Serikali kupitia fedha
za mfuko wa jimbo ilichangia shilingi 600,000 sawa na asilimia 2.6 na Shule ya
Msingi Ngana kupitia fedha za ruzuku ikachangia Shilingi 534,000 sawa na
asilimia 2.3.
Alisema kwa Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa
katika Shule ya msingi Lubele uliogharimu Jumla ya Shilingi 14,756,500 mchango
wa Kampuni hiyo ni Shilingi 9,821,000,wananchi kupitia nguvu kazi Shilingi
4,352,000,Diwani Shilingi 682,000 na madhehebu
mbalimbali ya dini Shilingi 201,000.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo,Makalla
aliwataka wakazi wilayani hapa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Kampuni
hiyo kwakuwa inaonyesha jitihada nzuri za kuboresha miundombinu ya Elimu.
“Ukibebwa uwe tayari kutoa ushirikiano.Hawa
wanaendelea kutuchangia kwakuwa na ninyi mmekuwa mstari wa mbele kushiriki
katika utekelezaji wa miradi inayoanzishwa kwenye maeneo yenu.Lakini pia hili
ni fundisho kuwa kama watu wa kutoka mataifa mengine wana utayari wa kuchangia
maendeleo ya kumkomboa mtoto wa hapa Kyela kielimu kwa nini wewe mtanzania wa
haapa ugome?”
“Lakini ni muhimu pia kutambua kuwa
kinachotukutanisha na wadau hawa ni zao la Cocoa.Sasa ni wakati kwetu kutambua
kuwa zao hili lina faida hivyo tuhakikishea tunalima zaidi ili siku zijazo hawa
washawishike kuja kujenga kiwanda japo cha kuchakata zao hili katika hatua za
awali hapa kwetu”alisisitiza Makalla.
Post a Comment