Header Ads


MKURUGENZI WA MANISPAA YA UBUNGO NDUGU JOHN KAYOMBO AFANYA ZIARA MAENEO YA MANZESE


Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John L. Kayombo

DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Kayombo tangu ateuliwe na Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli amekuwa na desturi ya kutembelea wananchi waliopo katika eneo lake la kiutawala ili kusikiliza kero zao na kuzitatua mara moja siku ya jana tarehe 09/02/2017 alipotembelea kata ya Manzese ili kusikiliza kero za wananchi na kujionea maeneo ya wazi yaliyovamiwa nakuona namna ya  kuyapatia ufumbuzi  wake.

Katika muendelezo wa hilo hapo jana, amedhuru maeneo anuai  akiongozana na wataalamu kutoka Manispaa anayoiongoza  ili kuweza kujionea, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi yakiwemo maeneo ya wazi yaliyovamiwa katika kata ya Manzese kwa lengo la kuyarudisha serikalini na kuonana na wahusika pamoja na wapangaji. 

Katika ziara yake Mkurugenzi alianza kwa kutembelea ofisi za kata ili kusikiliza kero za wananchi na watendaji kwa ujumla.
“Nimekuja hadi huku kwa sababu sitaki taarifa za kuletewa ofisini nataka nijionee mwenyewe kwa macho yangu, lakini pia lazima tufahamu Serikali ya awamu ya tano ni ya tofauti” Alisema Kayombo.   

 “Lazima kuwe na ufuatiliaji na uwajibikaji kwa kila mtumishi kwa nafasi yake kwa wananchi wake wote hadi katika ngazi ya mtaa, mapato ya serikali yamekuwa yakipotea sana na kuna watu wamehodhi maduka kwa muda mrefu bila ulipaji kodi unaoeleweka wala mikataba inayoeleweka, Watu wengine wameenda mbali hadi kufikia hatua ya kuvamia maeneo ya wazi,Tupo kwa ajili ya kufuatilia na kutatua”. Alisistiza Kayombo

Baada ya kusikiliza kero na changamoto Mkurugenzi Kayombo aliamua kutembelea katika maeneo yote yenye kero ili kujionea hali halisi.
Katika eneo la pembezoni mwa Shule ya  Msingi Manzese, Mkurugenzi alimwamuru fundi seremala aliyevamia eneo la wazi aondoke kabla ya tarehe 30/03/2017 kwani amekuwa alifanya shughuli zake kinyume cha sheria na bila kufuata utaratibu* na fundi seremala aliridhia makubaliano hayo.
Katika mtaa wa Tupendane ambapo kuna frame 14 ambazo zimejengwa katika eneo la wazi, Mkurugenzi alitoa agizo la wamiliki wote wa maduka kufika ofisini kwake  Kibamba CCM siku ya Jumatatu tarehe 12/02/2018 kwa ajili ya mazungumzo. 

Vile vile Mkurugenzi Kayombo aliwataka wapangaji wote waliopangishwa maduka kutokulipa tena pesa au kodi ya aina yoyote kwa mtu yoyote. Pia alowaomba wafike siku hiyo hiyo na mikataba yao ya upangishwaji ili kufikia muafaka na kufanya maamuzi ya mwisho. Wazo hilo lilipokelewa na pande zote kwa utekelezaji 

Katika mtaa wa Mnazi Mmoja karibu na soko la urafiki ambapo kuna choo cha Umma ambacho Manispaa hakifaidiki nacho kutokana na kutokukusanya mapato, Mkurugenzi aliamuru choo hicho kifungwe mara moja. Aliagiza hivyo sio tu kwa sababu Manispaa inakosa mapato lakini pia kwa sababu choo hicho kinavujisha maji machafu na ni hatari kiafya kwa wananchi wa eneo hilo. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mnazi Mmoja kwa kushirikiana na Mtendaji waliahidi kuyasimamia maagizo hayo ya Mkurugenzi.

Ziara ya Mkurugenzi ilimalizika katika Mtaa wa Muungano ambapo kuna eneo la wazi yaani Open space ambalo limevamiwa na kuna ujenzi unaoendelea na unafanywa na mtu aliyefahamika kwa jina la Chuwa.
Lakini pia kuna wafanyabiashara ambao nao wamejenga frame15 katika eneo la wazi. Mkurugenzi pia aliwataka wale wote ambao wapo kwenye orodha ya uvamizi kufika ofisini kwake siku ya Jumatatu sawia na wale wa mitaa mingine. 

Mkurugenzi pia aliuzuia Uongozi wa soko la Manzese kuendelea kuchangisha michango kwa ajili ya ujenzi wa soko. Aliwaambia kuwa ujenzi wote utasimamiwa na Manispaa na wananchi wanaona kama umechelewa lakini mpango wa Halmashauri ni kujenga kwa awamu mbili. Aliwahakikishia wananchi wa Manzese kuwa ujenzi utakuwa ni wa kisasa na anawaandalia eneo zuri la biashara na ndio maana ametoa fedha za mapato ya ndani Tshs milioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo kwa awamu ya kwanza.

Mkurugenzi aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ipo kwa ajili yao na itarudisha maeneo yote yaliyovamiwa. Aliwaomba wananchi na watendaji wote kwa ujumla kubadilika na kupiga kazi.
Wananchi walimpongeza Mkurugenzi kwa utendaji wake wa kazi uliotukuka na kuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha katika kila sekta. Hii ni kutokana na utofauti wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo wa kuwafikia wananchi na kutatua kero zao kwa usahihi na kwa wakati na kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano ya Mh. Dr John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tuu.

Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Ubungo

No comments

Powered by Blogger.