MTIBWA SUGAR YASHINDWA KUONYESHA UBAVU WAKE KWA SINGIDA UNITED
Mechi tano za raundi ya nane ligi kuu soka Tanzania bara zimemalizika huku Mtibwa Sugar ikishindwa kupaa kileleni baada ya kulazimishwa sare tasa na Singida United.
Mtibwa Sugar imelazimishwa sare hiyo kwenye uwanja wake wa nyumbani hivyo kushindwa kukaa kileleni baada ya kufikisha alama 16 na kulingana na timu za Simba, Yanga na Azam FC.
Mechi nyingine za jana ni ile kati ya Kagera Sugar dhidi ya Ndanda FC ambapo Kagera Sugar imepata ushindi wake wa kwanza baada ya mechi 7, ikishinda mabao 2-1. Lipuli FC imeshinda mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC.
Njombe Mji ikiwa nyumbani imelazimishwa sare tasa na Stand United huku Majimaji ikitoka sare ya bao 1-1 na Mwadui FC. Kesho kutakuwa na mchezo mmoja wa kukamilisha raundi ya nane kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Ruvu Shooting.Nafasi tano za juu kwenye msimamo zinashikiliwa na Simba yenye alama 16 ikifuatiwa na Yanga SC, Mtibwa Sugar na Azam FC zenye alama 16 pia. Singida United wanashika nafasi ya tano wakiwa na alama 13. Nafasi tatu za chini zinashikiliwa na Majimaji FC, Ruvu Shooting na Stand United zenye alama 5.
Post a Comment