FATMA KARUME NA MTOTO WA CHAHCHA WANGWE KUFUNGUA KESI
TAASISI
tatu zinazojihusisha na utetezi wa sheria na haki za binadamu,
zitafungua jumla ya kesi 10 ndani ya miezi mitatu katika Mahakama Kuu ya
Tanzania, kupinga zilichodai sheria kandamizi zinazominya demokrasia na
uhuru wa kujieleza.
Taasisi
hizo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
(THRDC).
Baadhi
ya sheria ambazo zimeanza kupambana nazo kwa kufungua kesi ili
zifanyiwe marekebisho, zimesema, ni Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya
Jeshi la Polisi na Sheria ya Uchaguzi.
Wakizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, viongozi wa taasisi
hizo walisema tayari wameshafungua kesi mbili katika Mahakama Kuu na
kwamba kesi nane zitafunguliwa baada ya miezi miwili.
Walisema
kesi hizo zimefunguliwa na wapiga kura wawili, Bob Chacha Wangwe na
Allan Bhujo watakaowakilishwa na mawakili kutoka taasisi hizo tatu.
"Tayari
tumeshafungua kesi mbili katika mahakama kuu, na kesi zingine nane
tutazifungua miezi miwili ijayo na kufanya jumla ya kesi kuwa 10,"
alisema Fatma Karume kutoka TLS.
Akizungumza
katika mkutano huo, Karume alisema wamejiandaa kuzipinga sheria hizo
alizoziita kandamizi, kwa mustakabali wa Watanzania.
"Hatutakata
tamaa kwenye hili," alisema Karume. "Tumeshuhudia vitendo vingi ndani
ya nchi vinavyowanyima wananchi demokrasia na uhuru wa kujieleza.
"Hii ni kinyume na katiba na ndiyo maana tumeunganika kupinga sheria hizo kwa mustakabali wa taifa."
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Anna Henga, alisema haki ya kukusanyika, kujieleza ni haki ya kila Mtanzania.
Post a Comment